"Wanyanyasaji huwa watu wema zaidi duniani" Lilian Nganga azungumza baada ya madai ya dhuluma ya Avril

Mkewe Juliani alidai kuwa wanyanyasaji wengi huwa wema kwa watu wengine isipokuwa watu wao wa karibu.

Muhtasari

•Katika taarifa yake fupi, mama huyo wa mvulana mmoja alitoa maoni yake mawili makuu kuhusu mahusiano yenye dhuluma.

•Lilian alisema suala la wanawake kuwatetea waume zao huwapeleka kwenye uhusiano wa kiwewe ambao hawawezi kujiondoa kwa urahisi.

Image: INSTAGRAM// LILIAN NGANGA

Mke wa rapa Juliani, Lilian Nganga ametoa maoni yake kuhusu unyanyasaji kwenye mahusiano, siku chache tu baada ya mwanamuziki Judith Nyambura maarufu Avril kujitokeza hadharani na kuibua madai ya kudhulumiwa kimwili na mzazi mwenzake J Blessing.

Katika taarifa fupi kwenye ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa mvulana mmoja alitoa maoni yake mawili makuu kuhusu mahusiano yenye dhuluma.

Katika maoni yake ya kwanza, alidai kuwa wanyanyasaji wengi huwa wema kwa watu wengine isipokuwa watu wao wa karibu.

"Kutokana na hadithi za sasa za ndani na kimataifa kuhusu unyanyasaji, mawazo yangu ni ... 1. Wanyanyasaji ndio watu wema zaidi ulimwenguni, ISIPOKUWA tu kwa wale walio karibu nao," Lilian Nganga alisema katika taarifa yake Ijumaa asubuhi.

Pia alisema kuwa suala la wanawake kuwatetea waume zao huwapeleka kwenye uhusiano wa kiwewe ambao hawawezi kujiondoa kwa urahisi.

"Wanawake kwa kweli huwalinda wanaume, na kuishia katika vifunngo vya kiwewe ambavyo huwa vigumu sana kujinasua," alisema.

Aliongeza, "Namtakia kila mtu anayepitia unyanyasaji ujasiri na uponyaji ili kuvunja mwendo huo. Jua litawaka tena.”

Kauli ya mke huyo wa zamani wa aliyekuwa Gavana wa Machakos, Alfred Mutua inajiri wakati ambapo taifa bado linaendelea kujadili madai ya unyanyasaji ya hivi majuzi yaliyoibuliwa na mwimbaji Avril dhidi ya mpenzi wake wa muda mrefu J Blessing.

Image: INSTAGRAM// LILIAN NGANGA

Siku ya Jumanne jioni, Avril alizua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wake baada ya kushiriki picha za kutisha za uso wake wenye alama za kupigwa na akaonekana kudokeza kuwa J blessing alikuwa amemvamia na kumpiga. Alikuwa ametumia akaunti ya Instagram ambayo amezima kwa sasa kufichua hali yake.

Baadaye, mama huyo wa mvulana mmoja alijitokeza kujitetea na kueleza kwa nini alifikia hatua ya kufunguka hadharani kuhusu yale aliyokuwa akipitia faragha.

Moyo wangu ni mzito sana hivi  ilinibidi kuuambia ulimwengu mambo yangu. Ndiyo, niliona kejeli kuhusu mimi kustahili kila kitu ambacho nimepitia enzi za uhai wangu na nina hakika kutakuwa na kejeli zaidi, lakini pia niliona jumbe za upendo na usaidizi." Avril alisema.

Mwanamuziki huyo ziadi aliweka wazi kuwa amemsamehe J Blessing kwa lolote lililotokea kati yao na pia kuwataka mashabiki wake wamsamehe mzazi mwenzake huyo.

Katika utetezi wake, J Blessing alidai kuwa moja ya picha alizochapisha mzazi mwenzake huyo ni tukio lililotokea mwaka jana.

Hata hivyo, alikiri kuwa hapo awali walikuwa na ugomvi uliopelekea vita, na kusababisha majeraha kwa wote wawili ambayo yalitibiwa hospitalini.

“Jana usiku (Jumanne) kulitokea hali iliyosababisha ugomvi, lakini haikuwa kipigo kama ilivyopendekezwa. Ninataka kumhakikishia kila mtu kwamba sikumpiga. Mimi si mnyanyasaji, na sikumpiga. Mimi ni binadamu ambaye nilifanya makosa katika maisha yangu." alisema.

Mtayarishaji huyo pia alitangaza kuwa yeye na Avril wamekubali kuishi tofauti baada ya tukio la hivi majuzi lililowahusu.