Zari achukua hatua kali baada ya picha zake chafu kusambazwa

Zari amekatisha mkataba na hoteli ya kifahari ambapo alikuwa mapumzikoni na mpenzi wake Shakib Cham.

Muhtasari

•Zari alivunja uhusiano wake na Divine Resort & Spa baada ya mpiga picha mmoja wa hoteli hiyo kukiuka kifungu cha mkataba.

•Pia aliizuia hoteli hiyo dhidi ya kutumia picha zake na mpenzi wake kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii au tovuti yao.

Zari Hassan na mpenzi wake Shakib Cham.
Image: HISANI

Mwanasoshalaiti Zari Hassan amekatisha mkataba wake na hoteli moja ya kifahari ambapo alikuwa mapumzikoni na mpenzi wake Shakib Cham.

Zari alivunja uhusiano wake na Divine Resort & Spa iliyo Uganda baada ya mpiga picha mmoja wa hoteli hiyo kukiuka kifungu cha mkataba wao kilichosema kwamba picha na video zote zinapaswa kuidhinishwa naye kabla ya kuachiwa.

"Mpiga picha huyo ameweka picha za Zari kabla ya kuidhinishwa. Kuanzia sasa, Zari hatabanwa tena na mkataba huo na hatatag  Divine Resort and Spa kwenye chapisho zake zozote za mitandao ya kijamii," sehemu ya barua ya Kusitishwa kwa Mkataba ambayo ilifikia Radio Jambo ilisoma.

Katika barua hiyo, mpenzi huyo wa zamani wa staa wa Bongo Diamond Platnumz alitoa agizo kwa mpiga picha mhusika kufuta picha zake zote alizochapisha kwenye kurasa zake na zile ambazo alituma kwa wanablogu.

Pia aliizuia hoteli hiyo dhidi ya kutumia picha zake na mpenzi wake kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii au tovuti yao.

"Kukosa kuzingatia yaliyo hapo juu kutahitaji timu kuendelea na hatua za kisheria na fidia," Barua hiyo ilisoma.

Katika video aliyopakia kwenye Snapchat, Zari alidai kuwa mpiga picha huyo alivunjisha picha hizo kwa sababu alitaka kuwa wa kwanza kutangaza habari za likizo yake na mpenzi wake kwenye blogu yake.

Alilalamikia hatua hiyo na kusema  kuwa mhusika alikosa weledi katika kazi yake na kukiuka makubaliano kati  yake na hoteli.

"Baadhi ya picha hizo ni nzuri na zingine kidogo ni PG 13," alidokeza.

Picha kadhaa za mwanasoshalaiti huyo akijivinjari na mpenziwe mdogo zimekuwa zikienea kwenye mitandao ya kijamii siku chache ambazo zimepita.

Baadhi ya picha ambazo haziwezi kuchapishwa kwenye tovuti hii zinaonyesha maudhui ya mapenzi. Wanamitandao ambao wamefikiwa na picha hizo wamekuwa wakitoa hisia mseto kuhusu  mahusiano ya wapenzi hao.

Mapema wiki hii taarifa mpya zilibuka kuwa mwanasoshalaiti huyo amekuwa akichumbiana tangu alipotengana na Diamond. Shakib mwenyewe, kupitia akaunti yake ya Tiktok alifichua kuwa wamekuwa wakisukuma mapenzi yao kwa miaka minne.

"Miaka minne pamoja..🥂❤ #Wanandoa #Hadithiyamapenzi," alisema chini ya video ya kumbukumbu zao pamoja.

Katika video hiyo, kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 alionekana akiwa amemshika Zari walipokuwa wakiingia ndani ya klabu.