Zari afurahia muda na ex wake, Diamond mwezi baada ya kufunga ndoa na Shakib

Video ya mwasosholaiti huyo ilionekana kumwangazia zaidi mzazi huyo mwenzake.

Muhtasari

•Mkutano wa wahusika wa Young Famous and African ni mara ya kwanza kabisa wa wapenzi hao wa zamani kukutana baada ya Zari kuolewa na Shakib.

•Zari na Shakib walifunga ndoa ya Kiislamu almaarufu Nikkah mwezi uliopita baada ya kuchumbiana kwa takribani mwaka mmoja.

wamehusika katika Young Famous and African 2
Diamond na Zari wamehusika katika Young Famous and African 2
Image: HISANI

Sehemu ya pili ya filamu ya Young Famous na African inayosubiriwa kwa hamu inaonyeshwa leo, Mei 19 kwenye Netflix.

Mastaa maarufu kutoka mataifa mbalimbali ya bara Afrika akiwemo mwimbaji wa Tanzania Diamond Platnumz na mzazi mwenzake Zari Hassan, rapa Nadia Nakai, muigizaji Khanyi Mbau, Naked DJ, Swanky Jerry, Kayleigh Schwark, 2Baba na Annie Idibia wamehusika katika sehemu ya pili ya filamu hiyo.

Siku ya Ijumaa, Zari aliwasherehekea wahusika wenzake wote huku akitangaza kuwa kipindi hicho kipeperushwa moja kwa moja kwenye Netflix nchini Afrika Kusini mwendo wa saa nne asubuhi.

"Tunapeperusha kuanzia saa nne asubuhi kwa saa za Afrika Kusini #YoungFamousandAfrican," alisema kwenye Instastori.

Aliambatanisha taarifa hiyo na video yake na wahusika wengine wote wakiwa wamekutana katika sehemu moja ambapo Diamond alioneka akiwa amesimama peke yake kwenye kona moja huku akifurahia kinywaji. Video ya mwasosholaiti huyo ilionekana kumwangazia zaidi mzazi huyo mwenzake.

Mkutano huo wa wahusika wa Young Famous and African huenda ukawa mara ya kwanza kabisa wa wapenzi hao wa zamani kukutana baada ya Zari kufunga pingu za maisha na mpenzi wake wa sasa Shakib Cham Lutaaya.

Zari Hassan na Shakib walifunga ndoa ya Kiislamu almaarufu Nikkah mwezi uliopita baada ya kuchumbiana kwa takribani mwaka mmoja.

Wawili hao walivishana pete usiku wa manane kuamkia Jumatatu katika hafla ya faraghani ambayo ilihudhuriwa na idadi ndogo ya watu.

Katika picha na video hafla hiyo iliyofanyika chumbani ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, wapenzi hao walionekana wamevalia Kiislamu kabisa huku wote wakiwa wameketi kwenye mkeka uliotandikwa sakafuni.

Shakib alionekana akiinama kwa goti moja na kumvisha Zari pete ya ndoa kwa furaha kabla ya wawili hao kupigana mabusu huku watu wachache waliohudhuria hafla hiyo wakiwasherehekea kwa makofi.

Vyanzo vya habari kutoka Uganda vilidai kwamba baada ya kuvishana pete katika tukio la faraghani, wawili hao ambao wamekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka minne waliweka Nikkah yao bayana kwa wazazi wa Zari.

Mwanasosholaiti huyo kutoka nchini jirani ya Uganda alitengana na Diamond mwaka wa 2018 baada ya kuchumbiana miaka kadhaa na kubarikiwa watoto wawili pamoja, Tiffah Dangote na Prince Nillan.