Harmonize ajawa wasiwasi kuhusu mahusiano yake akijiandaa kutembelea nchi ya ex wake, Briana

"Mungu anilinde na penzi changu hii safari isije kuwa mwanzo wa matatizo," Konde Boy alisema.

Muhtasari

•Harmonize alibainisha kuwa  anakoelekea ni nchi ya nyumbani ya mmoja wa wapenzi wake wa hivi majuzi, Brianna Jai.

•Hata hivyo hakufichua iwapo ana mpango wa kukutana na mrembo huyo wa Australia ambaye aliachana naye mwaka jana.

Harmonize na Briana
Harmonize na Briana
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Baada ya kutumbuiza katika miji kadhaa nchini Marekani, staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize anaelekea Australia ambako anatarajiwa kufanya shoo katika miji ya Sydney, Adelaide, Perth na Melbourne mwezi ujao.

Wakati akitangaza kuhusu ziara yake ya Australia kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumanne asubuhi, alibainisha kuwa  anakoelekea ni nchi ya nyumbani ya mmoja wa wapenzi wake wa hivi majuzi, Brianna Jai.

Kufuatia hayo, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alimuomba Mungu aingilie kati ziara hiyo isilete matatizo katika mahusiano yake.

"Australia ni mahali atokako Brianna!! Mungu anilinde na penzi changu hii safari isije kuwa mwanzo wa matatizo," Konde Boy alisema.

Aliongeza "Juni 9 Sydney, Juni 10 Adelaide, Juni 11 Perth, Juni 16 Melbourne, kateni tiketi zenu naja."

Hata hivyo hakufichua iwapo ana mpango wa kukutana na mrembo huyo wa Australia ambaye aliachana naye mwaka jana.

Harmonize alitangaza kutengana na Briana Machi mwaka jana kabla ya kuanza juhudi za kufufua uhusiano wake na Kajala.

Wakati huo, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alieleza kuwa aliachana na Briana kufuatia sababu kadhaa ikiwemo kuwa bado alikuwa na hisia za mapenzi kwa muigizaji Kajala, ambaye alikuwa ametengana naye wakati huo.

“Kuhusu Briana sina Tatizo nae kabisa, ni mtu mzuri ila hatuko pamoja, sababu nambari moja, nilimwambia nimetengana na mtu bila kugomabana na nampenda sana. Sasa sina uhakika kama nimemove on, lolote linaweza kutokea maana," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram mwishoni mwa mwezi Machi.

Pia alifichua kuwa aliachana na mwanamitindo huyo kutokana na tofauti za mawazo. Alisema walitofautiana kuhusu nchi gani ya wao kuishi huku kila mmoja akipendelea kukaa katika nchi yake ya kuzaliwa.

Huku akithibitisha kutengana kwao, Briana alimtakia kila la heri mwimbaji huyo na kufichua kwamba alikuwa amerejea  nyumbani kwao Australia.

“Kwa sasa nipo nyumbani Australia. ni kweli tumeachana na Harmonize namtakia kila laheri maishani mwake. Nashukuru kwa wale wote walionisupport nilipokuwa Tanzania nawapenada wote na kwa hayo nitarudi kuwatembelea tena. Inshallah,”  alisema.