Karen Nyamu ajibu kwa hasira baada ya kukosolewa kwa kuwapa wanawe jina la Samidoh

Nyamu alibainisha kuwa hajaribu kudhibitisha jambo lolote kwa mtu yeyote.

Muhtasari

•Huku mashabiki kadhaa wakithamini mwonekano wa watoto hao wawili, baadhi walimkosoa kwa kuwapa jina la Samidoh.

•Nyamu aliweka wazi kuwa hawezi kuingilia kati ya watoto wake na baba zao licha ya uhusiano  kati yake mwenyewe na wao.

wakati wa mazishi ya shemeji ya DP Rigathi Gachagua mnamo Februari 23, 2023.
Seneta Karen Nyamu na Samidoh wakati wa mazishi ya shemeji ya DP Rigathi Gachagua mnamo Februari 23, 2023.
Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Seneta maarufu wa kuteuliwa, Karen Nyamu, alipandwa na mori baada ya baada ya baadhi ya wanamitandao kumkashifu kwa kuwapa watoto wake wawili wadogo jina la baba yao, Samuel Muchoki almaarufu Samidoh.

Wikendi, mama huyo wa watoto watatu alichapisha picha nzuri ya wanawe, Sam Junior na Taraya Wairimu na kuwasherehekea kwenye mtandao wa Instagram. Pichani, wawili hao walionekana wenye muungano mzuri.

“Mazungumzo haya yalikuwa mazito, unadhani walikuwa wakitumia lugha gani,” aliandika Nyamu chini ya picha aliyoichapisha.

Mwanasiasa huyo aliambatanisha ujumbe wake na hashtag #Muchokis, kumaanisha kuwa ni watoto wa Muchoki (Samidoh).

Huku mashabiki kadhaa wakithamini mwonekano wa watoto hao wawili, baadhi walimkosoa kwa kuwapa jina la Samidoh.

"Lakini Karen ni mchokozi alafu watoto watrolliwe aanze kulia mwathiriwa hapa yet yeye ndio apost hashtag za kipuzi. Hua anajaribu kuprove point na watiti," mtumizi mmoja wa Instagram alimwambia Nyamu.

Huku akijibu, seneta huyo aliweka wazi kuwa hana nia ya kujaribu kudhibitisha jambo lolote kwa mtu yeyote.

"Hehehe woiye ukiskia umechokozwa na surname ya watoto wewe uko na kashida na huwezi saidika, na ukweli huwa haiproviwi dadangu. iriswariris," alijibu.

Mtumiaji mwingine wa Instagram alimkosoa Nyamu na kumwambia kwamba atajuta kuwaita watoto wake jina la baba yao.

Nyamu ambaye alionekana wazi kughadhabishwa na maoni ya shabiki huyo aliweka wazi kuwa kamwe hawezi kuingilia kati ya watoto wake na baba zao licha ya uhusiano uliopo kati yake mwenyewe na wao.

"Hehehe, ni sababu wewe ni mama mjinga. Huwa siingilii kati ya watoto wangu na baba zao bila kujali hali yetu.Utambulisho wao haubadiliki, huwezi kamwe kuhariri mizizi.  Ati nibadilishe jina la mtoto wangu wa kwanza kwa sababu siko tena na baba yake lol. Woiyee, kwani uliachwa aje," alijibu seneta huyo.

Wiki iliyopita, Nyamu na mzazi mwenzake Samidoh walisherehekea siku ya kuzaliwa ya binti yao mdogo kwa jumbe maalum.

Samidoh alimtaja bintiye kama mdogo wake na kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa akiadhimisha kutimiza mwaka mmoja.

Nyamu alichapisha picha za kupendeza za sherehe ya siku ya kuzaliwa ya bintiye na kuelezea upendo wake kwake. 

"Mtoto wangu wa bottom-up ametimiza mwaka mmoja! Naam, binti mfalme, utawala wako juu ya ufalme wa mioyo yetu umefikia mwaka mzima, na ulionekana kuwa malaika kabisa leo kwenye sherehe zako za kuzaliwa. Una akili, wewe ni mjuvi, na umekusudiwa ukuu, mtoto wangu," aliandika.

Karen pia aliwashukuru marafiki na familia yake kwa kuungana nao ili kumsherehekea binti yake.