Mamake Steven Kanumba abariki ndoa ya aliyekuwa mkwewe, Wema Sepetu na Whozu

Bi Mutegoa alieleza kuwa wakati akichumbiana na Kanumba, Wema Sepetu alikuwa na tabia nzuri.

Muhtasari

•Akizungumza kwenye mahojiano, mamake Kanumba alibainisha kuwa muigizaji huyo ni mwanamke mzuri ambaye amelelewa vizuri.

•Alibainisha kwamba kabla ya mwanawe kufariki zaidi ya mwongo mmoja uliopita, alikuwa na urafiki mkubwa na Wema Sepetu.

Wema Sepetu, Steven Kanumba na Whozu
Image: HISANI

Bi Flora Mutegoa, mama ya aliyekuwa staa wa filamu bongo, marehemu Steven Kanumba amemimina sifa kemkem kwa aliyekuwa mpenzi wa mwanawe, Wema Sepetu.

Akizungumza kwenye mahojiano na Msasa Media, mamake Kanumba alibainisha kuwa muigizaji huyo ni mwanamke mzuri ambaye amelelewa vizuri.

"Nawashukuru sana wazazi wake. Walimlea katika misingi imara. Haya mambo mengine ni ujana tu, lakini kwenye nidhamu na heshima, walimlea vizuri sana," alisema Bi Mutegoa. A

Alibainisha kwamba kabla ya mwanawe kufariki zaidi ya mwongo mmoja uliopita, alikuwa na urafiki mkubwa na Wema Sepetu. Alieleza kuwa wakati akichumbiana na Kanumba, muigizaji huyo alikuwa na tabia nzuri.

"Kuna wengine akija pale yuko katika kuchokonoroa kucha, lakini Wema hayuko hivyo. Akija nyumbani anabadilisha nguo, kama unafanya hivi anaingia yeye mwenyewe anafanya. Sio akifika miguu nne, TV na kucha. Wema hayuko hivyo," alisema.

Mama Kanumba alifichua kwamba  muigizaji huyo alikuwa akimpikia sana huku akibainisha kuwa anastahiki kuwa mke bora.

Alibainisha kwamba Wema Sepetu hajawahi kumkosea kwa namna yoyote ile na ameendelea kudumisha uhusianoa mzuri naye. Kufuatia hayo, alimtakia mafanikio mazuri maishani ikiwa ni pamoja na ndoa yake na Whozu.

"Namshukuru na namuombea kwa Mungu mambo yake yakafanikiwe.. kila kitu na mtu yeyote, awe Whozu sijui nani, Mungu ambariki. Mimi kwangu Wema hajawahi kunikosea hata siku moja," alisema Mamake Kanumba.

Takriban mwaka mmoja uliopita, Wema Sepetu aliadhimisha miaka kumi tangu kifo cha  Steven Kanumba.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Wema alifufua kumbukumbu zake na mwigizaji huyo kwa msururu wa picha.

Wema ambaye pia amewahi kuwa kwenye mahusiano na Diamond alimtakia marehemu mapumziko mema peponi.

"Siwezi kuamini mwongo umepita.. Mwongo hivo tu.. Rest Easy Booboo," Wema aliandika chini ya picha zake na Kanumba.

Wema na Kanumba walichumbiana kwa kipindi kisichothibitishwa kabla yao kutengana katika hali tatanishi.

Katika kipindi cha mahusiano yao, Wema alipata ujauzito mara mbili na  kila mara kuutoa, jambo ambalo anaamini limemwathiri hadi wa leo. Takriban miaka mitatu iliyopita, alikiri kuwa kuavya mimba ya kwanza ilikuwa ni makubaliano kati yao ila ya pili ilifanywa kwa siri bila Kanumba kujua.

Kanumba alifariki mnamo Aprili 12, 2012. Kwa wakati huo alikuwa anachumbiana na mwigizaji Elizabeth Michael ambaye alishtumiwa kuhusika na kifo chake na kushtakiwa kwa kosa la jaribio la mauaji.