Ahsanteni nyote, nisingeweza pekee yangu - Luludiva

Muhtasari

• Muigizaji na msanii kutoka Tanzania, Luludiva amepelekea katika ukurasa wake wa Instagram kuwashukuru wote waliompa bega kipindi mamake mzazi aliaga dunia.

• Akiwa ndo mtoto wa pekee, Luludiva amekiri kwamba mapenzi yake kwa mamake yalikuwa mazito na hivyo itamchukua muda mrefu kukubali kwamba hatamuona tena kipenzi chake.

Luludiva
Luludiva
Image: Instagram KWA HISANI

Muigizaji na msanii kutoka Tanzania, Luludiva alizamia ukurasa wake wa Instagram kuwashukuru wote waliompa bega kipindi mamake mzazi aliaga dunia.

Ametoa shukrani zake za dhati kwa mashabiki wake na serikali kwa mchango waliotoa wakati ambapo alikuwa anapitia kipindi kigumu kwa kumpoteza mtu ambaye alikuwa msingi wa maisha yake.

Hii ni kwa kila mmoja aliejitoa juu yangu kwa hali na mali, Wasanii wenzangu, Viongozi mbalimbali, Vyombo vya habari, Wadau tofauti, Mashabiki zangu, ndugu, jamaa marafiki na Watanzania wote walioguswa kwa ujumla, iwe kwa kuja kuniona, kwa kunipigia simu, kwa kusafiri na mimi, kwa post za faraja na kwa namna yoyote ile, kutoka moyoni mwangu kabisa nawashukuru sana sana WOTE na NINATHAMINI ,”’ aliandika Luludiva.

Akiwa mtoto wa pekee, Luludiva amekiri kwamba mapenzi yake kwa mamake yalikuwa mazito na hivyo itamchukua muda mrefu kukubali kwamba hatamuona tena kipenzi chake.

Luludiva pia hajakosa kushukuru kampuni zote anazoshirikiana nazo kibiashara kwa kusimama naye kidete mpaka wakati mipangilio ya safari ya mwisho ya mamake ilipokamilika.

Kulingana naye, amekuwa akijifungia ndani tangu kuondokewa na mzazi wake huyo kutokana na uzito wa tukio hilo ila amesema kwamba ameamua kukubali hali kwa kuwa Mungu ndiye hutoa na ndiye hutwaa.