Mcheshi Cartoon Comedian ashambuliwa, kunani?

Muhtasari

• Mchekeshaji maarufu wa kike nchini Kenya Cartoon Comedian amezua madai ya kushambuliwa na watu anaowataja kuwa walitumwa na mtu ambaye alimpasha kwamba hana talanta ya ucheshi.

• Yaani juu tu ya kusema mtu hana mistari ndio wanitumanishie watu wanipige. Ni haki lakini?

Cartoon Comedian
Image: Facebook

Mchekeshaji maarufu wa kike nchini Kenya Cartoon Comedian amezua madai ya kushambuliwa na watu anaowataja kuwa walitumwa na mtu ambaye alimpasha kwamba hana talanta ya ucheshi.

Akiongea kwenye mkanda wa video aliyoipakia kwenye kurasa zake mitandaoni, Cartoon anadai kwamba siku chache zilizopita alisema kwamba msanii fulani hana kipaji cha na kuwa analazimisha tu, jambo ambalo anadai lilipelekea msanii huyo ambaye hajamtaja kwa jina kumtumia wahuni ili kumdhuru.

“Yaani juu tu ya kusema mtu hana mistari ndio wanitumanishie watu wanipige. Ni haki lakini? Juzi tu nimesema mtu hana kipaji, sasa amenitumia watu waniharibu sura. Si vizuri hata kidogo. Ni wakati sasa wasanii tuache kuwa na ujinga,” Cartoon alisikika akilalama.

Siku mbili zilizopita Cartoon alipakia picha mtandaoni na kuzifuatisha na maneno kwamba “Mabosi wa kikweli hawalazimishi talanta. Na msiseme nimetaja ‘mapenzi tight’”

Inadaiwa alikuwa anampasha mtu fulani katika Sanaa ya burudani nchini, ambaye baadae alikuja kujibu mipigo kwa kumtumia wahuni wampige.

Anadai kwamba ni heri mara kumi msanii huyo angemfuata chemba ili amsihi amsaidie kumuandikia mistari badala ya kumtumia wahuni, kwani talanta yake yeye ni asilia na si kulazimisha.

“Heri angeniita tuongee ningemsaidia kuandika mistari, hii talanta yangu ni asilia,” alisema

Sehemu inayochekesha katika video hiyo ni mahali huyo mchekeshaji anasema kwamba alitumiwa wahuni ambao hawakuja na zana za kuogofya na hapo akamshauri mbaya wake wakati mwingine akimtumia wahuni, ahakikishe amewekeza katika wahuni wenye zana za kutisha.

“Wakati mwingine ukituma wahuni, hakikisha wana zana za kutisha. Sasa hao walikuja na tochi ndio walinipiga nayo. Heri hata wangekuja na bunduki ingeniogofya. Wekeza katika majambazi wako bwana,” alisema

Je, unahisi madai haya ni ya kweli ama Cartoon anajaribu kutafuta kiki tu mitandoni kama ilivyo kawaida ya wasanii wengi nchini?