Chimano wa Sauti Sol azungumzia maana ya mapenzi kwake

Muhtasari

• Mwanamuziki wa kundi la Sauti Sol, Chimano amezungumzia maana ya mapenzi katika Maisha yake kwa mara ya kwanza tangu kutangaza wazi kwamba yeye ni shoga.

• Mapenzi au upendo ni kielelezo cha usafi. Mapenzi hayabagui, mapenzi ni suluhu la matatizo mengi tuliyo nayo hapa duniani - alisema Chimano

chimano
chimano

Mwanamuziki wa kundi la Sauti Sol, Chimano amezungumzia maana ya mapenzi katika Maisha yake kwa mara ya kwanza tangu kutangaza wazi kwamba yeye ni shoga.

Msanii huyo ambaye anaendelea kushirikiana na shirika la habari la Radio Afrika katika tamasha za shirika hili anatarajiwa kupiga tamasha kubwa Zaidi ambalo amelibatiza kwa jina ‘Love & Harmony’

Akihojiwa na Mpasho, Chimano alifunguka kuhusu maana ya mapenzi kwake na akasisitiza sababu halisi za kusambaza mapenzi haswa mwezi huu wa mapenzi

“Mapenzi au upendo ni kielelezo cha usafi. Mapenzi hayabagui, mapenzi ni suluhu la matatizo mengi tuliyo nayo hapa duniani kwani unapoanzia kwenye mapenzi huwa tayari unaanzia kwenye hatua ya kusikiliza na kutaka kumuelewa mtu mwingine. Mapenzi hayana masharti, huo ndio upendo kwangu. Inajumuisha yote, unapompenda mtu, ni kumbatio halisi muda wote. Wacha tupendane,” Chimano alisema

Msanii huyo aligonga vichwa vya habari na mitandaoni kwa sana mwishoni mwa mwaka jana baada ya kujitokeza wazi na kukiri kwamba yeye ni mmoja kati ya kundi la LGBTQ, kundi linalojulikana kote duniani kama la mashoga, wasagaji, wenye jinsia Zaidi ya moja na watu wasio wa kawaida.

Watu waliibua maoni kinzani kuhusu hatua yake hiyo ya kukiri kuwa shoga, baadhi wakimpongeza kwa ujasiri wa kukiri jambo hilo ambalo limetapakaa katika jamii lakini wengi huogopa kulizungumzia huku wengine wakimuapiza kwa kushabikia ushoga jambo ambalo Wafrika wengi wanalitaja kama ni la wazungu.

Mnamo Februari 26, Chimano anatarajiwa kuongoza tamasha la Love and Harmony katika maeneo ya Two River akishirikishwa na wanabendi wenzake kama Bien Aime Baraza na Nviiri the Storyteller.