Majambazi waua polisi kisha kuiba bunduki mbili na chakula Isiolo

Muhtasari

•Kwa kawaida kituo hicho huwa na maafisa tisa lakini kulikuwa na maafisa wawili tu wakati wa uvamizi.

•Baada ya kuua afisa, majambazi hao waliingia kituoni na kuiba bunduki mbili pamoja na chakula kabla ya kutoweka.

crime scene
crime scene
Image: MAKTABA

Genge la majambazi waliokuwa wamejihami walivamia kituo kimoja cha polisi cha katika kaunti ya Isiolo na kuua polisi mmoja kabla ya kutoroka na bunduki mbili aina ya G3.

Tukio hilo linaripotiwa kutokea mwendo wa saa moja usiku wa Jumatatu.

Mamlaka ya polisi imesema kwa kawaida kituo hicho huwa na maafisa tisa lakini kulikuwa na maafisa wawili tu wakati wa uvamizi.

Konstabo Francis Njeru alipigwa risasi kichwani na kufariki papo hapo kabla ya majambazi hao kuingia kituoni na kuiba bunduki mbili pamoja na chakula kisha kutoweka.

Polisi wanashuku majambazi hao walikuwa wametoka katika kaunti jirani na walipanga kuiba silaha za kutumia katika uvamizi mwingine.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba kimoja cha kuhifadhi maiti cha kaunti hiyo ya Isiolo.

Eneo hilo limekuwa likishuhudia changamoto nyingi ikiwemo ukame na mashambulizi ya kijambazi katika kipindi cha miezi kadhaa ambacho kimepita.

Msemaji wa polisi Bruno Shioso amesema wanaendelea kuwasaka majambazi hao na ili kuwafungulia mashtaka. Aliongeza kuwa wanakusudia kurejesha silaha zilizoibwa.