Ukichunguza wafisadi Kenya, utakutana na mauti au mahakamani - Jane Mugo

Muhtasari

• Malkia wa upelelezi Jane Mugoh alitiririkwa na machozi mahakamani kwa kile alichokidai kwamba waliomteka nyara bado wamo ndani ya mahakama hiyo na kudai kwamba maisha yake yamo hatarini.

• Amasema masaibu yake yanatokana na kusema kwamba atawania uwakilishi wa kina mama katika kaunti ya Kirinyaga.

Jane Mugo
Image: Facebook

Mpelelezi binafsi, Jane Mugoh alizua vimbwanga katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi Februari 1, alipofika kwa ajili ya kusikizwa kwa kesi ya kutishia maisha ya mfanyabiashara.

Jane ambaye alidai kuwa yeye ni mpelelezi wa kibinafsi alitiririkwa na machozi kwa kile alichokidai kwamba waliomteka nyara bado wamo ndani ya mahakama hiyo na kudai kwamba Maisha yake yamo hatarini.

Baadae akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, aliteta kuwa masaibu yanayomuandama yanatokana na azma yake ya kutaka kuwania uwakilishi wa kike katika kaunti ya Kirinyaga.

“Pindi baada ya kutangaza kuwania nafasi ya siasa, mashtaka bandia yalilimbikizwa dhidi yangu. Mashtaka hayo yaliibuliwa na polisi pamoja na majambazi ambao niliwahi kupeleleza mwaka wa 2015,” Mugoh aliandika.

Jane Mugo
Image: Facebook

Mugoh alisema kuwa waliokusudia kuhujumu azma yake ya kuwakilisha wanawake kaunti ya Kirinyaga walileta wanahabari ambapo mmoja wao alisema waliitwa na wapelelezi wa DCI.

“Hapa Kenya, unafanya upelelezi kuhusu mafisadi na kinachofuata ni wewe kupatikana ukiwa umefariki, au unajikuta mahakamani. Mimi hata ingawa nimeumizwa kimwili, lakini niko imara kiroho,” aliandika Mugoh.

Kwa kile anachosema ni kulengwa kisiasa, Mugoh anashangaa kama kweli hii ni Kenya ambayo rais alitangaza kupiga vita ufisadi.

“Wale mnaobweka bure kwa njia hasi ni kwa sababu hamjui nini kinachoendelea. Nilitegemea mtasema tu wakati nitaleta ushahidi wangu. Nawaombea Maisha marefu ili mshuhudie baraka zangu,” aliandika Mugoh.

Baada ya kumalizika kwa sarakasi hizo mahakamani, Mugoh alisema kwamba anaelekea kusikojulikana kwa ajili ya ibada na maombi, wakiwa na familia na marafiki wa karibu.