Presenter Ali azungumzia tofauti kati ya Kenya na Tanzania

Muhtasari

• Presenter Ali amefunguka mengi kuhusu tofauti alizoziona kati ya sanaa ya Kenya na Tanzania, anasema Kenya watu bado hawajakubali sanaa kama Tanzania.

Presenter Ali
Image: Facebook

Mtangazaji Presenter Ali ambaye pia anajiongeza kama mkuza maudhui wa mitandaoni amerejea nchini baada ya kuwa na ziara ya kutafuta majhojiano na mastaa mbalimbali nchini Tanzania kwa takribani wiki mbili hivi.

Mtangazaji huyo akihojiwa na Mungai Eve amezungumza mengi na haswa kuhusu tofauti katika masuala mbalimbali baina ya vile yanavyofanyika na kuchukuliwa nchini na Wakenya, tofauti na vile yanavyofanyika nchini Tanzania.

Baadhi ya tofauti ambazo alizungumzia ni jinsi Watanzania wanawachukulia wasanii wao, michezo yao na hata uandaaji wa hafla na tamasha nchini Tanzania ni tofuati kabisa na nchini Kenya.

Akitolea mfano uandaaji wa tamasha na hafla za kutumbuiza, Presenter Ali alisema kwamba kulingana na yeye na kile alichoona na kuhisi akiwa nchini Tanzania ni kwamba wale wanawapenda na kuwathamini sana wasanii wao na huwa wanawapiga sapoti ya kikweli wanapoandaa tamasha.

Ali alisema kwamba kwa mfano msanii Marioo wa Tanzania kwao kule si msanii mkubwa kihivyo lakini ana uwezo wa kuandaa tamasha na ukumbi ukafurika furifuri tofauti na jinsi wasanii wa Kenya kwa mfano Khaligraph Jones ambaye ni msanii mkubwa nchini akiweka tamasha kwenye ukumbi wa KICC hauwezi ukajaa mashabiki jinsi ambavyo Marioo atajaza Tanzania.

Alisema hili lipo Kenya kwa sababu hatupendi wasanii wetu na ni nadra sana kupata Wakenya wakiwa sapoti wasanii wa humu nchini haswa katika kuhudhuria tamasha kama hizo.

Ali pia alisema kwamba wasanii wengi wa nchini Tanzania wako na uongozi unaofanya kazi sana na takribani kila msanii ana meneja wa kazi zake za muziki na wanaheshimu sana mameneja wao, tofauti na huku Kenya ambapo asilimia Zaidi ya tisini kwenda mbele ya wasanii hawana uongozi wa kazi zao za miziki, wengi huwa wanakipiga kijeshi la mtu mmoja na kupelekea wengi wao kudhulumiwa au kulaghaiwa kwa kutojua jinsi ambavyo muziki unafaa kusimamiwa.

Alisema wasanii wa Tanzania wanaheshimu sana mameneja wao kiasi kwamba kama meneja amemkataza kutoshiriki katika kitu chochote kama kufanya mahojiano kwa sababu labda anajiandaa kuachia albamu au muziki mpya, wale huwasikiza lakini hapa Kenya msanii aliyebahatika kuwa na meneja anaweza akaambia asionekane kila sehemu kirahisi rahisi tu na kufanya mahojiano lakini kwa sababu mtu fulani ni rafiki yake na amemuita kwa mahojiano, msanii huyo atakaidi maagizo ya meneja ya kufika kwa mahojiano hayo.

Hilo ndilo kubwa ambalo linaathiri Sanaa ya Kenya kwa sababu wasanii wenyewe hawana mameneja na wachache walio nao hawana heshima kwa mameneja wao, na ndio maana wengi huishia kulaghaiwa na ‘cartels’.

“Wasanii wa Kenya unapata sana hawana respect ya management in TZ unapata they really respect management. Unapata yes wewe ndiye unamlipa meneja lakini huyu meneja anaelewa sana brand yako in such a way that akikuambia leo huwezi fanya interview, hata humuulizi kwa nini. Mimi nilienda kule kutafuta interviews na wasanii wengi na nilipatana nao lakini wengi walikuwa ready kusaidia kufanya interview but for one reason or another, hawako allowed na management,” alisema Presenter Ali.