Mtangazaji Jamal Gaddafi aondoka runingani ili kuangazia siasa

Muhtasari

•Jamal ametangaza kuondoka katika runinga ya KTN ili  kufanikisha ndoto yake ya kuwakilisha watu wa Malindi bungeni.

• Mtangazaji huyo wa kitengo cha burudani pia alisema kuwa analenga kuwania kiti hicho cha ubunge kwa tikiti ya  ODM.

Mwanahabari Jamal Gaddafi akiwa na Kinara wa ODM, Raila Odinga
Image: Jamal Gaddafi (Facebook)

Mtangazaji Jamal Gaddafi ametangaza kuondoka katika runinga ya KTN ili  kufanikisha ndoto yake ya kuwakilisha watu wa Malindi bungeni.

Gaddafi aliyasema haya katika kituo cha KTN alipokuwa akifanya kipindi chake cha mwisho kabisa mnamo Januari 29.

“Ni wakati wa kujaribu kitu kipya. Hii ni mara yangu ya mwisho kabisa kuonekana katika runinga ya KTN na hivi sasa nimefungua ukurasa mpya katika siasa. Imekuwa ni miaka minane yenye furaha,” alisema Gaddafi huku akilengwa na machozi

Akiwa kwenye mahojiano na Presenter Ali, Gaddafi alifunguka Zaidi ni kwa nini ameamua kujitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge Malindi.

“Watu wa Malindi kwa muda mrefu hawajapata mtu wa kuwatetea kule bungeni. Mimi nakuja kama mtetezi wa watu wa Malindi," aliongeza Gaddafi.

Mtangazaji huyo wa kitengo cha burudani pia alisema kuwa analenga kuwania kiti hicho kwa tikiti ya ODM na kuongeza iwapo atapoteza tikiti hiyo katika hatua ya mchujo, basi atajitosa ugani kama mgombea huru.

“Mwanzo nitapitia mchujo kujaribu bahati yangu katika kupata tikiti ya chama cha ODM lakini nikikosa nitamuunga mkono yeyote atakayeibuka mshindi ila azma yangu ya kuwa mbunge bado itasalia pale pale kwani nitawania kama mgombea huru,” alisema Gaddafi.

Kuondoka kwake kutoka runinga ya KTN kunaambatana na agizo la baraza la wanahabari nchini Kenya, MCK linalomtaka yeyote anayelenga kuwania nafasi ya siasa kujiondoa katika kitengo chochote cha uanahabari miezi sita kabla ya uchaguzi kufanyika.