Khaligraph Jones aachia albamu yake 'Invisible Currency'

Muhtasari

• Msanii wa rap nchini Kenya Khaligraph Jones ameachia albamu yake ya tatu chini ya miaka 9.

• Albamu hiyo ameipa jina 'Invisible Currency' ambapo amewashirikisha mastaa mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Khaligraph Jones
Image: Instagram

Staa wa mtindo wa kufoka almaarufu Hiphop nchini Kenya Khaligraph Jones ameachia albamu yake yenye tungo kumi na saba mnamo Jumatatu alasiri.

Albamu hiyo aliyoibatiza kwa jina ‘Invisible Currency’ ina ngoma 17 ambazo miongoni mwao amepiga collabo za nguvu na majina makubwa katika Sanaa ya muziki ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya wasanii wakubwa ambao amewashirikisha katika mradi huo mpya ni mfalme wa muda wote wa bongo fleva Alikiba, gwiji wa Ohangla Prince Indah, Rude Boy kutoka Nigeria, Blackway kutoka Ghana miongoni mwa majina mengine ya kistaa.

Staa huyo wa rap ameshabikiwa na wengi jinsi ambavyo ametaradadi vyema kabisa katika albamu yake hiyo huku akiwashirikisha wasanii kutoka ohangla, bongo fleva hadi rap ambapo ameitaja kuwa albamu yenye ubora wake na ambaqyo imesawazishwa vilivyo katika upande wa aina za miziki.

Jones alitoa albamu yake ya kwanza mwaka 2014 aliyoipa jina ‘Point of No Retun’ iliyofanya vizuri sana ikizingatiwa kwamba ndio ilikuwa albamu yake ya kwanza kabisa na miaka minne baadae akatoa albamu nyingine kwqa jina ‘Testimony 1990’ mwaka wa 2018 ambayo ndio albamu iliyomuweka katika nafasi nzuri kabisa ya umaarufu nje ya nchi.

‘Invisible Currency’ ni albamu yake ya tatu na ambayo tayari ngoma zote zinapatikana kwenye jukwaa la kupakua miziki la Boomplay.