Akothee kuvuna miti yenye thamani ya 400M baada ya kuchochewa na Rais Kenyatta

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano amesema kuwa anatarajia kila mti kumletea angalau shilingi 10,000.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee amesema rais Uhuru Kenyatta alimtia msukumo wa kuwekeza kwenye miti kutoka kwa rais Uhuru Kenyatta.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee amefichua kuwa miaka nane iliyopita alipanda miti 40,000 aina ya Eucalyptus Grandis nyumbani kwake Rongo  baada ya kusikiza ushauri wa rais.

Mama huyo wa watoto watano amesema kuwa anatarajia kila mti kumletea angalau shilingi 10,000.

"Nilijifunza kuhusu miti kupitia kwa Rais Uhuru Kenyatta, nilipata msukumo na kulitekeleza huko Rongo. Sasa nina miti 40,000 aina ya Eucalyptus Grandis . Hesabu 40,000 × 10000 pesa za Kenya. Hizo zote kwa benki. Miti hiyo ina miaka 8 sasa. Pesa zilizo kichwani mwangu hadi kwenye banki yangu," Akothee aliandika.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 41 aliambatanisha ujumbe wake na picha iliyoonyesha shamba kubwa ambalo amepanda miti hiyo.

Kando na uimbaji, Akothee pia ni mjasiriamali na mfanyibiashara shupavu. Anamiliki kampuni ya uchukuzi wa watalii kati ya biashara zingine.

Akothee pia ni balozi wa kampuni mbalimbali.