DJ Moh afichua ugonjwa uliopelekea mkewe Size 8 kulazwa hospitalini

Muhtasari

•Kanda ya video ilionyesha msanii huyo akiwa mdhaifu huku wahudumu wawili wa afya wakijitahidi kumzuia asianguke.

•Mwaka jana mama huyo wa watoto wawili alipoteza ujauzito kutokana na tatizo hilo la shinikizo la damu.

Image: INSTAGRAM// DJ MO

Mhubiri Linet Munyali almaarufu Size 8 Reborn anaendelea kuhudumiwa katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuugua.

Habari za kulazwa kwa mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili zilitangazwa kupitia ukurasa wake wa Instagram.

"Size 8 REBORN hatakuwa na mahubiri ya saa saba mchana leo kwa kuwa alilazwa hospitalini, tafadhali muwekeni kwenye maombi yenu na tunaomba kumuona akihubiri mtandaoni hivi karibuni," Tangazo hilo lilisoma.

Ujumbe huo uliambatanishwa na kanda ya video ambayo ilionyesha msanii huyo akiwa mdhaifu huku wahudumu wawili wa afya wakijitahidi kumzuia asianguke.

DJ Moh akizungumza na Mpasho amefichua kuwa mkewe alilazwa baada ya kukumbwa na shinikizo la damu.

"Alikimbizwa hospitali na kulazwa kutokana na shinikizo la damu, anaendelea vizuri zaidi sasa," DJ Moh amesema.

Mwaka jana mama huyo wa watoto wawili alipoteza ujauzito kutokana na tatizo hilo la shinikizo la damu.