Arrow Bwoy azungumzia uhusiano wake na Jalang'o baada yake kufichua ujauzito wao kabla yao

Muhtasari

•Arrow Bwoy alisema mgombeaji huyo wa kiti cha ubunge cha Lang'ata alijuta kitendo chake na kupiga hatua ya kuomba msamaha.

•Alisema mkewe alikuwa anakabiliana na matatizo kadhaa ya ujauzito ndiposa wakachelewesha tangazo lao.

Image: HISANI// ARROW BWOY, JALANG'O

Mwanamuziki Ali Yussuf almaarufu Arrow Bwoy ameweka wazi kuwa kwa sasa hakuna uhasama wowote kati yake na mchekeshaji Jalang'o.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Arrow Bwoy alieleza kuwa alimsamehe Jalang'o baada ya kuomba msamaha kwa kufichua habari za ujauzito wa Nadia.

Arrow Bwoy alisema mgombeaji huyo wa kiti cha ubunge cha Lang'ata alijuta kitendo chake na kupiga hatua ya kuomba msamaha.

"Jalang'o alijifunza, alituma ujumbe akiomba msamaha. Pia yeye anajua hakufanya poa ndio maana alitutafuta. Hatuna ugomvi. Hata hivo iwe funzo kuwa watu waheshimu mipaka ya wenyewe," Arrow Bwoy alisema.

Mwanamuziki huyo alisema yeye pamoja na kipenzi chake Nadia Mukami walikuwa wanasubiri wakati mwafaka kutangaza habari kuhusu ujauzito wa mtoto wao wa kwanza.

Alisema mkewe alikuwa anakabiliana na matatizo kadhaa ya ujauzito ndiposa wakachelewesha tangazo lao.

"Alichofanya Jalas si jambo nzuri, kila mtu anajua. Masuala ya familia ni ya familia pekee. Ujauzito ni suala nyeti. Wanawake ndio wanaijua sana. Hata mimi sikuwahi tangaza. Hata kama mimi ni mhusika nilikuwa nasubiri wakati ambao yeye ako tayari kuisema. Kuna mambo mengi,kuna dili alikuwa anakimbiza na pia hakuwa tayari kisaikolojia," Arrow Bwoy alisema.

Arrow Bwoy na Nadia Mukami walitangaza kuhusu ujauzito wao wa kwanza siku ya Jumanne wakati dunia ilikuwa inaadhimisha siku ya wanawake.