"Nilikuwa nimekufa siku 4" Akuku Danger asimulia mambo ya kutisha yaliyompata alipokuwa mgonjwa

Muhtasari

•Akuku amesema amekuwa akipata nafuu kutoka nyumbani baada ya kupewa ruhusa kutoka hospitali mwezi uliopita.

• Akuku amefichua kwamba  hakuwa anafahamu kabisa kilichokuwa kinaendelea kati ya mwezi Desemba na Februari kwani alikuwa amezima.

Magonjwa yaliyokuwa yameshambulia Akuku Danger yafichuliwa
Magonjwa yaliyokuwa yameshambulia Akuku Danger yafichuliwa
Image: INSTAGRAM// SANDRA DACHA

Mchekeshaji wa Churchill Show, Mannerson Ochien'g almaarufu Akuku Danger yumo safarini ya kupata afueni kikamilifu baada ya kuwa anaugua kwa takriban miezi mitatu mapema mwaka huu.

Akuku amesema amekuwa akipata nafuu kutoka nyumbani baada ya kupewa ruhusa kutoka hospitali mwezi uliopita.

"Nimekuwa nikipona pole pole kutoka nyumbani. Nguvu imerejea, niko karibu kuanza kazi. Tuanze kazi sasa, tuchekeshe Wakenya," Akuku alisema akiwa kwenye mahojiano na Mpasho.

Mchekeshaji huyo alisimulia kwamba alipitia kipindi kigumu alipokuwa amekumbwa na matatizo ya kupumua kwa miezi hiyo mitatu.

Kuna kipindi ambapo alilazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kuzidiwa na ugonjwa. Ugonjwa wa pneumonia ambao ulikuwa umemshambulia ulimwathiri vibaya had kusababisha mapafu yake kuharibika.

Hata hivyo, Akuku amefichua kwamba  hakuwa anafahamu kabisa kilichokuwa kinaendelea kati ya mwezi Desemba na Februari kwani alikuwa amezima.

"Nilianza kukumbuka vitu mwezi Februari. Januari yote nilikuwa nimezima. Sikuuliza daktari mbona sikuwa nakumbuka vitu. Lakini akilini mwangu nilifikiria ni kwa sababu nilikuwa nimezima siku nne, nilikuwa nimefariki siku nne," Alisema.

Akuku alisema kwamba familia yake, marafiki na wasanii wengi wenzake walimtembelea hospitalini alipokuwa amelazwa. Alisema fahamu yake ilipotea tangu alipolazwa hospitalini mnamo mwezi Desemba.

"Hata singekumbuka nikiletwa hospitali. Kuna watu wengi ambao walikuja kuniona. Ningeona nyuso zao tu lakini sikujua wao ni kina nani. Kina Churchill na Terence walikuja lakini singeweza kuwatambua.. niliwaona baba yangu, dada zangu na kaka zangu lakini akilini nilikuwa najiuliza wao ni kina nani. Ilikuwa giza tupu!" Alisema.

Mchekeshaji huyo amewahakikishia mashabiki wake kwamba fahamu na nguvu yake imerejea na yupo tayari kuanza kutumbuiza tena.

Hata hivyo amefichua kwamba bado hajaweza kukamilisha kulipa bili ya hospitali kwani kuna salio la takriban shilinhi milioni 1.5.