"Jamani ndoa tamu!" Diva The Bawse ajigamba miezi miwili baada ya kufanya harusi

Muhtasari

• Diva The Bawse alidai kwamba anazidi kunawiri kutokana na mahaba anayopokea kutoka kwa mumewe.

•Mtangazaji huyo aliweka wazi kuwa mumewe kwa kawaida huwa haingilii kazi yake kwa namna yoyote ile.

Image: INSTAGRAM// DIVA THE BAWSE

Mtangazaji wa Wasafi Media Diva The Bawse ameweka wazi kwamba anaifurahia sana ndoa yake na Sheikh Abdulrazak Salum.

Diva na Sheikh walifunga pingu za maisha mwezi Machi katika harusi ya kufana iliyohudhuriwa na wanafamilia, marafiki na wasanii mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari, Diva alidai kwamba anazidi kustawi kutokana na mahaba anayopokea kutoka kwa mumewe.

"Jamani ndoa tamu. Niangalie. Nina amani na nina raha. Kumbe ni mume wangu, nafurahia ndoa," Diva alisema.

Diva hata hivyo amefichua kuwa  kwenye ndoa kumemfanya afanye marekebisho madogo kwenye mtindo wake wa maisha.

"Nguo nimebadilisha. Sivai sana nguo fupi. Lakini kichwa sivai mauchungi, mtanisamehe mimi ni Diva. Hizo vichungi sivai. Hata Abdul anajua, labda kama tunaenda msikitini Ijumaa ndio nitavaa. Kuna zile sehemu ambazo nikienda nitavaa lakini nikienda ofisini mimi ni Diva yuleyule," Alisema.

Mtangazaji huyo aliweka wazi kuwa mumewe kwa kawaida huwa haingilii kazi yake kwa namna yoyote ile. Abdul hata hivyo amemtambulisha Diva kwenye dini na kumfunza kusuali.

Abdul mwenyewe pia alizungumza na waandishi wa habari kupitia njia ya simu na kufichua jinsi anavyomdekeza mkewe na kufanya afurahie ndoa yao.

"Nampa mapenzi. Namuogesha kwa mate yangu, namlisha, namlaza, namchekesha," Bw Abdul alisema.

Alisisitiza kuwa mkewe anampa mahaba tele na kuweka wazi kuwa hana shaka kuhusu uaminifu wake.

"Diva ananiogesha. Walahi Bilahi. Ananipikia, ananitandikia, ananidekeza, ananikumbatia nikilala. Mi nageuka hivi ananikumbatia kwa nyuma mpaka asubuhi," Alisema.

Abdul pia aliweka wazi kuwa anakusudia kuishi maisha yake yote na Diva pekee na hana mpango wa kuoa mke mwingine.