Mulamwah: Mkiombea bei ya unga ishuke, kumbukeni kuombea pia SIMITI, CHUMA na MAWE

Muhtasari

• Mulamwah amewataka Wakenya kuombea bidhaa za ujenzi kupungua bei huku akiendelea na ujenzi wa nyumba yake kijijini.

Mchekeshaji Mulamwah
Facebook Mchekeshaji Mulamwah
Image: Mulamwah

Mchekeshaji maarufu nchini Kenya Kendrick Mulamwah amewataka Wakenya wanaonung’unika kutokana na bei za bidhaa muhimu haswa vyakula kupanda kuzidi kuomba bei zipunguzwe na pia akawataka wanapofanya hivyo wasisahau kuombea bei za nyenzo za ujenzi pia kupunguzwa.

Kupitia kwa instastories zake, Mulamwah alionekana kuungana na Wakenya kulalamikia maisha magumu kutokana na uchumi kuadhirika pakubwa na bei za bidhaa kupanda, ila yeye akawa analalamikia zaidi upande wa malighafi ya ujenzi kama vile simiti ya kutengeneza saruji na pia vyuma.

“Mkiombea bei ya unga ishuke, kumbukeni kuombea pia SIMITI, CHUMA na MAWE,” aliandika Mulamwah.

Mcheshi huyo ambaye miezi miwili iliyopita alidokeza kwamba anaanza ujenzi wa jumba lake la kifahari nyumbani kwao katika kaunti ya Trans Nzoia aliandika kwa malalamiko makubwa kwamba bidhaa hizo za ujenzi zimekuwa ghali mno kwa watu ambao wanafanya ujenzi.

Katika instastories zake, Mulamwah pia hakusita kuonesha picha za mwendelezo wa jumba lake hilo ambapo msingi ndio mwanzo unaisha na jumba kuanza kusimama.

Mchekeshaji huyo hakusita kuleta utani katika maneno yake ambapo alitania kwamba msingi wa jumba hilo lake umemgharimu kiasi kikubwa cha pesa ambazo ni sawa na gari zuri tu mtu anamiliki mahali fulani.

“Bidhaa hizo ni ghali kama nini! Msingi pekee ni kagari kazuri mahali,” alitania Mulamwah.

Ikumbukwe miezi michache iliyopoita mcheshi huyo alifichua kiini kilichosababisha mahusiano yake na aliyekuwa mpenzi wake Carrol Sonie kuvunjika ambapo alimrushia mpenziwe vijembe kwa madai kwamba alikuwa mtu wa kupenda starehe za maisha huku akijitetea vikali kwamba kwa upande wake alikuwa na fikira tofauti za kutaka kuwekeza zaidi na pia kujenga nyumba na si kubarizi katika starehe.

Malalamiko ya Mulamwah yanakuja kipindi ambapo Wakenya wengi wanazidi kuungulia makali ya mfumuko wa bei za bidhaa kama vile unga, mafuta ya kula, sabuni miongoni mwa bidhaa zingine ambazo zimepanda bei mara dufu.