"Sanaa yote ya burudani Kenya imekufa!" asema Eric Omondi

Omondi aliahidi kwamba sanaa itazidi kuwa kimya hadi Septemba atakaporudi kuichangamsha tena

Muhtasari

• “Kimya hiki chote katika Sanaa kinatokea tu kwa sababu rais yupo likizoni. Nilichukua likizo fupi ili tu kudhibitisha hili" - Eric Omondi

Mchekeshaji Eric Omondi
Image: Eric Omondi (Instagram)

Mchekeshaji Eric Omondi sasa anadia kwamba Sanaa ya burudani humu nchini imekufa kabisa na kuisha.

Omondi akiandika kwenye instastory yake, alidai kwamba Sanaa ya burudani kwa ujumla haina nguvu tena kwani ilishakufa kitambo sana hata kabla watu wagundue.

“Sanaa yote ya burudani imekufa kabisa na kutulia. Hakuna kitu kinaendelea; si muziki muzuri, si burudani, hakuna!” alisema Omondi.

Mchekeshaji huyo alisema kwamba haya yote yanatokea kwa sababu yeye yupo likizoni na hakuna mtu mwingine zaidi yake yeye anayeweza kuiburudisha na kuichangamsha Sanaa hiyo kama yeye, rais wa ucheshi Africa, anavyojiita.

“Kimya hiki chote katika Sanaa kinatokea tu kwa sababu rais yupo likizoni. Nilichukua likizo fupi ili tu kudhibitisha hili,” alijipiga kifua Eric Omondi.

Akionekana kuwakanyagia wasanii wenzake chini na kuonesha kwamba yeye ndiye mwenye thamani kubwa ya kuamua uwepo au mwisho wa Sanaa, Omondi alisema kwamab ni yeye tu ambaye amekuwa akiibeba Sanaa katika mabega yake mwenyewe na hakuna mtu mwingine anayeweza kuvivaa viatu vyake kwani ni vikubwa na kila anayejaribu kuvivaa basi vinampwerepweta.

“Mimi tu ndiye ninayeibeba Sanaa ya burudani katika mabega yangu na mgongo wangu. Na huo ndio ukweli tusibishane!” aliandika Omondi.

Baadhi ya watu wanaofanya kweli kwenye Sanaa ya burudani kwa ujumla walifurika hapo na maoni tofauti tofauti ambapo wengi walimkashfu kwa kujiona kama yeye ndiye kuweza sana hali ya kuwa hana lolote.

Katika picha za mazungumzo ambazo Omondi alizipakia, alionekana kujibizana na shabiki mmojaq aliyemwambia kwamba yeye ndiye haoni wala kujua ni nini kinaendelea katika Sanaa kwa sasa.

“Wewe pekee ndio unaona kama hakuna kitu kinaendelea. Watu wako kazi bana. Ni wazi kwamba hujui miziki yenye inazungumziwa kwa sasa, watu wanafanya ziara katika vyuo vikuu, wanajinyakulia mikataba ya ubalozi katika kampuni za bidhaa mbalimbali lakini wewe hauoni,” mmoja alimwambia.

Omondi alibisha kauli hiyo huku akisema kwamba baadhi ya miziki ambayo inafanya vizuri mpaka sasa hivi ni miziki iliyotoka mwaka jana na mpaka sasa hakuna mziki wa kufurahisha ambao umetoka. Alimalizia akisema kwamba Wakenya wasubiri arudi kwenye Sanaa mwezi Septemba baada ya uchaguzi mkuu ndio watambue kwamba Sanaa inamtegemea yeye na si vinginevyo.

Je, unakubaliana na maoni ya Omondi?