"Huwa nalia siku zingine" Willis Raburu akiri kumfikiria bintiye miaka miwili baada ya kufariki

Adana alifariki wakati aliyekuwa mkewe Marya Prudence alikuwa akijifungua mnamo Desemba 31, 2019.

Muhtasari

•Raburu amefichua kuwa siku zingine huwa anajipata akilia anapomkumbuka bintiye ambaye alifariki punde baada ya kuzaliwa.

•Baby Adana,  alifariki wakati aliyekuwa mkewe  Marya Prudence alikuwa akijifungua mnamo Desemba 31, 2019.

Image: INSTAGRAM// WILLIS RABURU

Mtumbuizaji maarufu Willis Raburu amekiri kwamba machungu ya kumpoteza mwanawe bado yanamsumbua hadi leo.

Raburu amefichua kuwa siku zingine huwa anajipata akilia anapomkumbuka bintiye ambaye alifariki punde baada ya kuzaliwa.

Katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram, shabiki mmoja alimuuliza mtangazaji huyo wa Citizen TV ikiwa bado huwa anamkumbuka bintiye.

"Bado unamfikiria mtoto Adana?" Shabiki alimuuliza Raburu.

Alijibu, "Siwezi kusahau kamwe. Ni maumivu ambayo bado yananitoa machozi siku fulani. Ni yale ambayo unashughulika nayo siku moja baada ya nyingine. Moja ambayo huwezi kusahau. Yuko juu akiwafanya watu wengi wacheke,"

Bintiye mtangazaji huyo , Baby Adana,  alifariki wakati aliyekuwa mkewe  Marya Prudence alikuwa akijifungua mnamo Desemba 31, 2019.

Image: INSTAGRAM// WILLIS RABURU

Mwaka jana, wakati akiadhimisha miaka miwili baada ya kifo cha bintiye ya kuzaliwa na vilevile kufariki kwa bintiye, Raburu alisema anatamani sana angekuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa pamoja naye.

Alikiri kwamba tangu Adana alipoaga huwa anapatwa na mchanganyiko wa hisia kila mwisho wa mwaka  kwani hajui ikiwa anapaswa kusherehekea mwanzo wa mwaka mpya ama kuomboleza bintiye.

"Heri ya miaka 2 ya kuzaliwa Adana. Malaika wangu. Ninakufikiria kila wakati ninao. Ninakukumbuka na uso wako mzuri. Sitasahau kwani muda ule nilikuwa nawe katika chumba baridi na hata busu langu halingeweza kukurudisha hai! Nadhani hiyo inafanyika katika hadithi za hadithi tu. 😔💔 Nilipaswa kuwa nikisherehekea hatua zako muhimu lakini badala yake nimekaa hapa nikionea malaika wivu kwa sababu wanapata kuwa nawe kila siku.

Siku zote  kama hii ni siku ngumu kwa sababu sijui kusherehekea mwaka mpya au kuomboleza. Najua ungetaka tukusherehekee na ndio maana niko hapa. Piga kelele nyingi mbinguni leo wajulishe wazazi wako ni akina nani! 😢 Nakupenda. Mama na baba watakupenda milele na milele! 🙏🏾💔❤️😇" Aliandika.

Kwa sasa mtangazaji huyo anatarajia mtoto wa pili na mke wake wa sasa, mwimbaji Ivy Namu kutoka Uganda.

Wachumba hao walitangaza ujauzito wa pili takriban miezi miwili iliyopita kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

Mwaka jana wawili hao walibarikiwa na mtoto wa kiume.