(+video) Daddy Owen aeleza sababu ya kuvalia gumboots katika mazishi ya Ngashville

Owen alisema ndio mara ya kwanza kutumbuiza jukwaani akiwa amevalia gumboots.

Muhtasari

• "Niliimba hata kwa gumboots kwa mara ya kwanza!!! Sote hapa tulimfahamu @ngashtheartist kwa nafasi tofauti,” Owen alifafanua.

Jumamosi ilikuwa ni siku ya kiza kinene cha huzuni na simanzi katika tasnia ya Sanaa ya injili Kenya, katika msiba wa msanii Ngashville.

Daddy owen ambaye amekuwa akimuomboleza Ngash tangu kifo chake kuwekwa wazi wiki jana alionekana kwenye mazishi hayo akiwa amevalia gumboots huku akiwaongoza wasanii wengine na waombolezaji kusherehekea maisha ya Ngash na kumpa buriani.

Owen baadae alifafanua zaidi juu ya uvaaji huu usio wa kawaida kwake haswa kwenye hafla za mazishi na kusema kwamba kuvaa kwake gumboots halikuwa jambo la ghafla bali ni kitu ambacho alifika kwenye msiba akiwa ameratibu akili yake kuhusu matokeo ambayo yangehitaji mkono wake.

Msanii huyo maarufu kwa vibao wa kumtukuza Mungu alisema kwamba ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kuvalia gumboots na kushiriki kutumbuiza kwenye jukwaa.

Pia alisema maana yake kubwa ya kuvaa gumboots ni kwa sababu alikuwa anajua fika angehitajika kushika jembe na kushiriki katika uchimbaji kaburi la kumlaza Ngashville kama njia moja ya kutoa heshima zake za mwisho kwake.

“Nilivalia gumboots sababu nilijua nitashika jembe na koleo la kutupa mchanga wakati wa kumzika rafiki yangu.. nilikuja nimejiandaa. Niliimba hata kwa gumboots kwa mara ya kwanza!!! Sote hapa tulimfahamu @ngashtheartist kwa nafasi tofauti,” Owen alifafanua.

Wasanii wakiongozwa na Daddy Owen walitumbuiza katika msiba huo kwa nguvu zote huku akisema kwamba Ngash alikuwa siku zote ni mtu aliyependa furaha na iliwalazimu kusherehekea maisha yake.