"Umekaa kama Waititu aliyesema tusogeze mito!" Ombija azomea kwa kutetea kelele za vilabu

Ombija alikuwa anateta kwamba waliokuwa wakilalamika kuhusu kelele ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wakaazi wote.

Muhtasari

• Mwaka 2018, Waititu alisema kuwa mito iliyo karibu na majengo yake haramu inapaswa kusogezwa ili kuzuia kubomolewa. Mnamo 2022 Trevor Ombija anasema kwamba tunapaswa kuzuia sauti kwa nyumba zetu - Odangaring alisema.

Trevor Ombija asutwa
Trevor Ombija asutwa
Image: Facebook

Baada ya diwani wa Kileleshwa Robert lai kuanzisha mchakato wa maeneo ya kujistarehesha kufungwa jijini kwa kuweka kelele nyingi zisizoweza kudhibitika, sasa wamiliki wa maneno hayo ya burudani wamejitokeza kujitetea.

Mwanahabari wa runinga Trevor Ombija ambaye ni mmoja wa wamiliki wa klabu moja mtaani Kilimani ambayo imeshtumiwa kwa kuwapigia wakaazi kelele alionekana kweney klipu ya video akiteta vikali kwamba alipata malalamishi kutoka kwa watu, malalamishi amabyo kulingana na yeye hayakuwa na uzito wa kuweza kufungwa eneo lake la burudani.

Ombija alisema kwamba inafaa iwekwe kuwa sharia kuwa kama kuna kelele inaathiri watu basi wengi wa watu hao wawe ndio wanateta na si wachache kama ilivyokuwa katika muktadha huu.

Alisema hata alitaka kuweka vifaa vya kuzuia sauti katika makazi ya walalamishi ili kuwazuia kutoka athari za kelele za muziki ambazo walikuwa wanateta.

“Nimekuwa na maswala ya kujirudia mara kwa mara kulingana na viwango vya sauti vilivyopo. Jambo moja ambalo ningependa kupendekeza, na kama mwenyekiti alikwisha sema, kunapokuwa na malalamiko dhidi ya mwenye baa au mgahawa, tuwe na zaidi ya nusu ya watu wanaolalamika. Ikiwa nyumba ni 20, 15 kati yao watuonyeshe upangishaji wao, saini na utuambie hii ndio shida," Ombija alisema.

Matamshi haya yake yaliwapata watumizi wa mtandao wa Twitter kwa ghadhabu mno ambapo walimshtumu kwa kuwa na ujasiri wa kuteta hali ya kuwa yeye ndiye mwenye klabu ya kuwasumbua wakaazi kwa kelele.

Aliyekuwa rais wa chama cha waansheria nchini Nelson Havi alimjia juu kwa kumzima kwamba yeye ndiye mwenye kelele na badala ya kunyamaza apangwe bado ndiye anakuwa chiriku kuteta kote kote kuwa ameonewa.

“Trevor Ombija, ikiwa wewe ndiye mpiga kelele, unafunga mdomo wako. Huna sababu ya kutaka kuziba masikio yetu. Uchafuzi wa kelele lazima uzuiwe,” Havi alimzomea.

Wengine walifananisha madai haya yake na yale ya aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu aliyetaka mto kusogezwa kando badala ya kubomoa jumba lililokuwa limejengwa katika mkondo wa maji.

“Mwaka 2018, Waititu alisema kuwa mito iliyo karibu na majengo yake haramu inapaswa kusogezwa ili kuzuia kubomolewa. Mnamo 2022 Trevor Ombija anasema kwamba tunapaswa kuzuia sauti kwa nyumba zetu ili baa yake iendelee kuchafua vitongoji vyetu,” mmoja kwa jina Odangaring alisema.