Harmonize ajivunia baada ya kuibuka bora zaidi nchini Kenya na Tanzania

Bosi wa Kondegang ,Harmonize, ametwaa uongozi katika mataifa hayo mawili.

Muhtasari

•Katika orodha ya hivi punde kutolewa, wasanii wa Tanzania wanaongoza katika nchi yao na pia katika nchi jirani ya Kenya.

•Kwa kipindi kirefu sasa wasanii wa Bongo  wamekuwa wakishabikiwa sana hapa nchini zaidi ya wanamuziki wetu wa hapa nyumbani.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Chati za YouTube za wasanii bora zimetoka na ni wazi kuwa wanamuziki wa Bongo wanafanya vizuri kuliko wenzao wengine wa Afrika Mashariki.

Katika orodha ya hivi punde kutolewa, wasanii wa Tanzania wanaongoza katika nchi yao na pia katika nchi jirani ya Kenya.

Bosi wa Kondegang Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ametwaa uongozi katika mataifa hayo mawili katika orodha mpya.

"@youtubemusic yasema vile!!!!" Harmonize alijivunia ushindi huo kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na screenshot za orodha za wanaofanya vizuri zaidi kwenye YouTube nchini Kenya na Tanzania.

Zuchu na bosi wake Diamond Platnumz walichukua nafasi ya pili na ya tatu mtawalia nchini Tanzania huku staa mkongwe wa Bongo Alikiba akichukua nafasi ya nne. Barnaba, Marioo, Rayvanny, Msodoki Young Killer, Martha Mwaipaja na Ayra Starr  wa Nigeria walifunga orodha ya kumi bora Tz katika mpangilio huo.

Nchini Kenya, wasanii wa Bongo walinyakua nafasi za kwanza tatu huku wanamuziki Wakenya wawili tu wakipata nafasi katika orodha ya wasaniii kumi bora. Harmonize wa Kondegang aliibuka wa kwanza nao wasanii wa WCB  Zuchu na Diamond Platnumz wakachukua nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.

Malkia wa Afrobeats Ayra Starr aliibuka wa nne huku Rayvanny na Bura Boy wakichukua nafasi ya tano na ya sita mtawalia.

Willy Paul ndiye msanii Mkenya anayefanya vizuri zaidi kwenye YouTube hapa nchini baada ya kuorodheshwa wa saba. Mwenzake Bahati ni wa pili huku akichukua nafasi ya kumi katika orodha hiyo ambapo wanamuziki wa Nigeria  Ruger na Asake  wameibuka wa nane na tisa mtawalia.

Orodha ya wasanii bora kwenye Youtube nchini Kenya inaonyesha wazi kwamba aidha Wakenya wamelegea katika kuwaunga mkono wasanii wa nyumbani ama kuna jambo ambalo wanamuziki wa kigeni wanafanya zaidi ya wenzao wa hapa nchini. Kwa kipindi kirefu sasa wasanii wa Bongo hasa Diamond, Harmonize, Rayvannyy na Zuchu wamekuwa wakishabikiwa sana hapa nchini zaidi ya wanamuziki wetu wa hapa nyumbani.