Killy na Cheed wamshtaki Harmonize kwa kuwatimua Konde Gang

Wasanii hao walielekea kwenye bodi ya BASATA kutafuta haki kwa kile walisema mikataba yao ilivunjwa kwa njia tata.

Muhtasari

• Mapema wiki hii Msanii Harmonize alitangaza kuondoka kwa wawili hao katika lebo ya Konde Gang kwa kile alisema kwamba walihitimu.

Cheed na Killy wamemshtaki Harmonize BASATA
Cheed na Killy wamemshtaki Harmonize BASATA
Image: Maktaba

Siku chache baada ya kinara wa lebo ya Konde Music Worldide Harmonzie kuwaaga rasmi wasanii Killy na Cheed kutoka lebo hiyo, sasa utata na utashi zaidi umezuka.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vinaarifu kwamba wasanii hao wawili wanahisi walitimuliwa kwa njia isiyofaa na sasa wameanzisha mchakato wa kutafuta haki kupitia bodi ya sanaa nchini humo, BASATA.

Jarida la Mwananchi linaripoti kwamba BASATA iliutaka uongozi wa KondeGang kujiwasilisha katika ofisi hizo kujibu tuhuma hizo ila hawakuweza kutii wito huo na badala yake wakaingia mitini.

"Taarifa ambayo inaelezwa walitaarifiwa kwa njia ya barua pepe (email) lakini mpaka inafika saa nane mchana sio Harmonize wala meneja wake waliotokea katika kikao hicho ambacho kilipaswa kuanza saa sita mchana," Mwananchi waliripoti.

Meneja wa wasanii hao aliyejitambulisha kwa jina la Sats Sembe, alisema sababu ya wao kufikisha malalamiko yao Basata ni kupinga utaratibu wa kuvunja mkataba na wasanii hao ambapo alieleza kuwa hakuna barua yoyote ya maandishi waliopewa mpaka sasa.

Sembe alisema kwa kuwa waliingia lebo ya Konde kwa maandishi basi hata kuondoka wanapaswa kuondoka kwa maandishi, ili kesho isije kutokea sintofahamu katika masuala ya kisheria.

"Huko mbeleni hatujui hili suala litafika hapa, lakini kwa kuanzia tumeanzia kwa walezi wetu na wazazi wetu Basata ambao katika hali ya kawaida tusingeweza kuwaruka. Lakini kama ikishindikana hatua hii tutaeda hata mahakamani ambapo kote huku barua ya maandishi ni muhimu kama ushahidi kwamba wameachana na wasanii wetu,"  Sembe alinukuliwa katika video moja iliyopakiwa na Mwananchi YouTube.

Kabla ya kujiunga lebo ya Konde Music Worldwide, Killy na Cheed walikuwa chini ya lebo ya msanii Alikiba, Kings Music.