Kondegang ya Harmonize yawapoteza mastaa wawili

Harmonize aliema wawili hao waliondoka kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wa lebo.

Muhtasari

•Konde Music Worlwide ilisema imefikia makubaliano na mastaa Ally Kili Omari almaarufu Killy na Rashid Daudi Mganga almaarufu Cheed.

•Killy na Cheed walijiunga na Konde Music Worldwide mwaka wa 2020 baada ya kugura kwenye lebo ya Alikiba ya Kings Music Records.

Mastaa hao wa Bongo wameondoka kwenye lebo ya Konde Music Worldwide
Killy na Cheed Mastaa hao wa Bongo wameondoka kwenye lebo ya Konde Music Worldwide
Image: INSTAGRAM//

Usimamizi wa lebo ya Bongo ya Konde Music Worldwide umetangaza kuondoka kwa wasanii wake wawili.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Konde Music Worlwide ambayo inaongozwa na Harmonize ilisema imefikia makubaliano na mastaa Ally Kili Omari almaarufu Killy na Rashid Daudi Mganga almaarufu Cheed.

Harmonize aliweka wazi kuwa wawili hao waliondoka kutokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wa lebo.

"Wasanii hawa watakuwa wasanii huru na kuweza kufanya kazi na kuingia mkataba na kundi au mtu yeyote na kuendeleza kazi zao kwani tunaamini ni vijana wasanii wenye uwezo mkubwa wa kufanikiwa katika safari ya muziki," taarifa iliyotiwa saini na usimamizi wa Konde Music Worldwide ilisomeka.

Lebo hiyo ilibainisha haitahusika  na jambo lolote litakalohusisha wasanii hao kuanzia leo Oktoba 10, 2022.

"Tunapenda kuwashukuru Killy na Cheed kwa ushirikiano wao katika kipindi chote cha kuwa pamoja na tunawatakia mafanikio mema katika kazi zao hapo baadae," taarifa hiyo ilisoma.

Killy na Cheed walijiunga na Konde Music Worldwide mwaka wa 2020 baada ya kugura kwenye lebo ya Alikiba ya Kings Music Records.