Harmonize ashtumiwa kwa kununua mapenzi ya Kajala

Msanii huyo amedaiwa kumhonga mchumba wake Kajala Masanja ili apendane naye.

Muhtasari

•"Mapenzi hachaguliwi mtu ila hakuna kitu kibaya kama mapenzi kunuliwa. Mdogo wangu alinunua mapenzi sio kupenda," H-Baba alisema.

•Msanii huyo wa zamani wa Kondegang alisema mtu hatakiwi kuanza kwa kutumia pesa kabla ya kuingia kwenye mahusiano.

Harmonize na mchumba wake Kajala Masanja
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo Harmonize ameshtumiwa kwa kumhonga mchumba wake Frida Kajala Masanja ili apendane naye.

Aliyekuwa msanii wa Konde Music Worldwide H-Baba amedai kuwa bosi huyo wake wa zamani alinunua mapenzi.

"Mapenzi hachaguliwi mtu ila hakuna kitu kibaya kama mapenzi kunuliwa. Mdogo wangu alinunua mapenzi sio kupenda," H-Baba alisema katika mahojiano na waandishi wa habari.

Msanii huyo ambaye kwa sasa yuko WCB alibainisha kuwa bosi wake wa zamani alitumia pesa nyingi kumtongoza Kajala arudi.

Huku akimkosoa kwa hilo, H-Baba alisema kuwa mtu hatakiwi kuanza kwa kutumia pesa kabla ya kuingia kwenye mahusiano.

"Unapoanza penzi na kugonga basi wewe hujui kutongoza. Unatakiwa uingie kwenye mahusiano ndio uanze kuhonga,"  alisema.

Alibainisha kuwa yeye mwenyewe humhonga msichana aliyejitosa kwenye mahusoiano naye kwa nyumba na viwanja.

"Mimi sihangaiki kwa sababu nishawaandalia maisha mazuri na watoto wangu," alisema.

Licha ya mzozo wake na Harmonize, mwimbaji huyo alibainisha kuwa anampenda na kumheshimu sana Kajala.

Mapema mwaka huu Harmonize alitumia mamilioni ya pesa katika juhudi za kurejesha mahusiano yake na Kajala yaliyokuwa yamegonga ukuta mwaka uliopita. Wawili hao walikuwa wamekosana  Aprili mwaka jana huku Harmonize akidaiwa kujaribu kumtongoza bintiye Kajala, Paula na kumtumia picha za uchi.

Wengi walijitokeza kumkosoa bosi huyo wa Kondegang kwa kutumia fedha nyingi kumfurahisha Kajala ili akubali msamaha wake.

Harmonize hata hivyo alidhihirisha kuwa hajuti lolote na kusema anampenda sana muigizaji huyo. Alisema alikuwa akifanya hayo yote katika juhudi za kumuonyesha mama huyo wa binti mmoja jinsi alivyomuhitaji.

"Mimi ni hustler tu na napenda mwanamke wangu. Najaribu kuonyesha jinsi ninavyohitaji arudi maishani mwangu!! Sio eti najigamba," alisema.

Juhudi za mwimbaji huyo hatimaye zilifua dafu kwani wawili hao walifufua mahusiano yao na wamekuwa pamoja kwa miezi kadhaa.

Mahaba ya wasanii hao yameendelea kunoga kila uchao huku wakionekana kuyafurahia sana maisha yao ya ndoa.