Kizz Daniel atumia nafasi ya shoo yake jukwani na kumtumia Davido ujumbe wa kihisia

Daniel alijisikia vibaya kutumbuiza jukwaani peke yake bila uwepo wa Davido.

Muhtasari

• Davido hajaonekana hadharani zaidi ya mwezi mmoja tangu kumpoteza mwanawe Ifeanyi.

• Kizz Daniel alisitisha shoo yake kwa dakika kadhaa akituma ujumbe wa hisia kwa msanii huyo ambaye bado anaomboleza kufiwa.

Kizz Daniel atuma ujumbe wa hisia kwa Davido
Kizz Daniel atuma ujumbe wa hisia kwa Davido
Image: Instagram

Mwimbaji maarufu Kizz Daniel ametuma ujumbe kwa nyota wa muziki na bosi wa lebo ya DMW, Davido, ambaye anaendelea kuomboleza mwanawe Ifeanyi, aliyeaga dunia mwezi Novemba.

Tangu kifo cha Ifeany, Davido amebaki nje ya mtandao na amekaa mbali na maonyesho ambayo alidaiwa kutumbuiza. Kizz Daniel katika chapisho alionyesha majuto kwamba mwimbaji huyo wa DMW hangeimba naye jukwaani kwenye tamasha lake la Abuja Jumapili, Desemba 11.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Kizz Daniel alipakia picha ya Davido na kumwambia kuwa anamkosa sana na kuwa wangefana sana pamoja jukwaani angekuwa bado katika hali na siha nzuri.

“Nakupenda ndugu yangu, nakukosa sana sio siri leo usiku tungefunika kabisa katika shoo yangu ya Abuja,” Kizz Daniel aliandika.

Davido tangu kifo cha mwanawe Ifeanyi katikati mwa mwezi Novemba, amekuwa mkinya sana ambaye hajakuwa akionekana mitanaoni na baadhi ya mashabiki wake wanahisi bado anaendelea kutatizika vikali kifikira na kimawazo.

Wengine wanamtaka Kizz Daniel kumpa shavu kwa niaba yao kwa vile yeye ako na ukaribu wa kumfikia ikilinganishwa nao.

“Tunamkosa Davido kusema kweli, natumai sasa anaendelea vizuri sasa japo dalili zote zinaonesha huyo jamaa anaumia na anapitia wakati mgumu sana. Tafadhali nyinyi marafiki zake mnafaa kuwa karibu naye muda wote kwa sababu sisi mashabiki zake hatuwezi kumfikia,” mmoja alimwambia Kizz Daniel.

“Najua tunaweza kuwa tunafikiri Davido anapona sasa hivi..lakini vipi kama hayupo ..iweje kama yuko chini kuliko hapo awali..huu sio utani tafadhali tunatakiwa kumuombea zaidi..Mungu akutie nguvu pale ulipo. nguvu zako zinaishia Davido,” mwingine kwa jina Breebytunx aliandika.