Christina Shusho hatimaye azungumzia kitendo cha Harmonize kuibusu miguu yake

Wawili hao walikutana nchini Kenya wikendi iliyopita kabla ya Harmonize kubusu miguu yake kwa kuinama chini.

Muhtasari

• Christina Shusho alimtaja Harmonize kama mwanake na kumtakia mema yatokayo kwa Mungu.

• Harmonize kwa upande wake alimuombea Shusho kufunikwa kwa damu ya Mungu siku zote.

Harmonize na Shusho
Harmonize na Shusho
Image: Instagram

Mwimbaji wa Injili kutoka Tanzania Christina Shusho hatimaye amevunja kimya kuhusu kitendo cha msanii wa nyimbo za dunia Harmonize kuinama chini na kubusu miguu yake.

Wawili hao walikutana Kenya, jijini Eldoret na Harmonize alifanya kufuru kwa kupiga magoti chini na kuibusu miguu ya Shusho kwa furaha huku akimtaja kama mtumishi wa Mungu mmoja ambaye ni wa kweli kuwahi kutokea.

Mengi yalisemwa kuhusu kipande hicho cha video baadhi wakisema kuwa Harmonize ana njama fiche ya kuvunja ndoa ya Shusho kwani kitendo hicho ni cha kimahaba zaidi.

Lakini Shusho ameamua kufunguka kuhusu video hiyo na kumtaja Harmonize kuwa kijana mwadilifu anayeipambania Sanaa ya Tanzania.

Alisema hivi karibuni atafunguka kwa kina kiini cha mazungumzo yao ambayo walikuwa nayo baada ya kukutana wote Kenya, japo kuwa kila mmoja alikuwa anafukuzia shoo yake tofauti.

Nikiwa Kenya kwenye huduma nilifurahi kukutana na Mtanzania mwenzangu Naye kaja kupeperusha bendera ya Tanzania nchini Kenya. Tuliyo Yaongea na @harmonize_tz ni story ya Siku nyingine. Mungu akubariki mwanangu,” Shusho aliandika.

Harmonize kwenye chapisho hilo alimshukuru Mwimbaji huyo kwa kuwa kielelezo bora huku akimtakia Mungu kumfunika kwa damu yake.

“Amen! Inshaallah! Damu Ya YESU Ikufunike!!” Harmonize alisujudu.