Huddah: Sina tatizo kuolewa kama mke wa 2 kwa mume mwenye utajiri kama King Solomon

"Kama unataka kuwa na wanawake zaidi ya mmoja, basi usiwe fukara na mjinga, angalau chagua moja" - Huddah.

Muhtasari

• Huddah aliwashauri wanaume wanaoparamia kuoa wanawake wengi ili kuiga Mflame Suleiman kwanza kutambua kuwa yeye alikuwa na utajiri.

Huddah atoa ushauri kwa wanaume wanaotaka wanawake wengi
Huddah atoa ushauri kwa wanaume wanaotaka wanawake wengi
Image: Instagram

Ikiwa wewe ni mwanaume mwenye mazoea ya kujilinganisha na mfalme Suleiman kutoka Biblia kuhusu uwezo wake wa kuwa na wanawake wengi, basi mwanasosholaiti Huddah Monroe ana ushauri kwako, vuta kiti ukae mkao wa kula.

Huddah amewasuta wanaume wenye mitazamo ya kuwa na wanawake wengi bila ya kuwa na utajiri wa kuwezesha kuendesha uhusiano wake miongoni mwa wanawake hao.

Ikiwa unadhani Mjasiriamali huyo wa bidhaa za kujipodoa hana weledi katika kubukua Biblia, basi umebofya namba tofauti.

Huddah aliwarudisha wanaume wa Aina hiyo kwenye Biblia na kuwakumbusha kuwa wanapojilinganisha na Mfalme Suleiman, mara nyingi huwa kuna sehemu wanaotea kuing’amua katika uwezo wake wa kumiliki wanawake wengi pamoja na michepuka.

Alisema kuwa kwa Suleiman kuwa na wanawake wengi, hakuwa maskini bali alikuwa ni tajiri mkubwa mwenye mali yake, lakini pia alikuwa ni mwingi wa busara – jambo ambalo wanaume wengi wanaojilinganisha naye katika kuwa na wanawake wengi, hawana!

Mwanasosholaiti huyo alisema hakuna mwanamke anayeweza kukataa kujiunga kwenye foleni ya wanawake wanaoolewa na mwanaume mmoja, ikiwa mwanaume huyo ni mkwasi na mwenye busara.

“Wanaume wanapenda sana kujilinganisha na mfalme Suleiman katika kuwa na wanawake wengi. Wanachokisahau ni kwamba yeye alikuwa Mflame, mwenye utajiri mkubwa pamoja na busara nyingi. Hata mimi nitakuwa katika foleni hiyo kwa mwanaume kama huyo. Kama unataka kuwa na wanawake zaidi ya mmoja, angalau basi usiwe fukara na mjinga, angalau chagua moja!” Huddah alishauri.

Huddah ambaye alidokeza kuwa ana miaka zaidi ya 30, alisema nadharia yake kuhusu wanaume wa Kiafrika bado ipo pale pale na haijapata kubadilika kwani taswira anayoiona kichwani mwake kuhusu wanaume wa Kiafrika haiwezi kumruhusu hata sekunde moja kuchumbiana na mmoja wa asili hiyo.