Diamond ampigia saluti Rayvanny kwa kuwekeza hela nyingi katika video ya 'Nitongoze'

Video hiyo ambayo Rayvanny aliachia Jumapili akimshirikisha Diamond ina wahusika zaidi ya 200, katika sehemu mbalimbali za kifahari.

Muhtasari

• Chini ya saa ishirini na nne, video hiyo tayari inakakribia watazamaji nusu milioni kwenye YouTube.

• Uwekezaji katika video hiyo unadhihirika wazi huku watu zaidi la 200 wakishirikishwa na wote wamepewa mavazi ghali na ya kipekee.

Diamond na Rayvanny
Diamond na Rayvanny
Image: Instagram

Wikendi iliyopita msanii Rayvanny kutoka lebo ya Next Level Music aliachia video ya wimbo wake mpya ‘Nitongoze’ akimshirikisha aliyekuwa bosi wake kutoka WCB Wasafi, Diamond Platnumz.

Katika video hiyo ambayo makuzi yanakisia uwekezaji mkubwa katika kila kitu, Diamond alimsifia Rayvanny kwa kufanikisha video hiyo ambayo watu zaidi ya 200 walihusika huku sehemu mbalimbali za kifahari zikitumika katika kufanya video yenyewe.

Diamond alimvisha koja la maua Rayvanny na kumpa hongera kubwa huku akisema kuwa anajihisi fahari kumlea na kuona akifanya mambo makubwa katika Sanaa hata baada ya kuondoka Wasafi na wengi kutoa utabiri wa kupotea kwake kama alivyotoweka Rich Mavoko baada ya kusepa WCB.

“#Nitongoze Video ya Rayvanny akimshirikisha Simba ishatoka sasa…Kaitizame kwenye bio ya @rayvanny … Hela umewekeza kwenye Video Chui, Ninajihisi fahari kuwa katika mradi huu wako kaka,” Diamond alisema.

Wasanii hao waliachia wimbo huo takribani miezi miwili uliopita na video yake imetoka wikendi hii ambapo mpaka sasa chini na saa ishirini na nne tayari imejizolea watazamaji zaidi ya laki nne kwenye jukwaa la kupakua video la YouTube.

Wimbo huo ambao kwa kiasi kikubwa una maudhui ya pombe ulisababisha majibizano makali kati ya Rayvanny na Harmonize wiki jana baada ya Kondeboy kutupa dongo kwa Rayvanny akisema si vizuri kwa wasanii kuachia nyimbo zenye maudhui ya vileo.

Harmonize alifanya chokoza ya maksudi kwa Rayvanny, jambo ambalo lilifanya waanze kutupiana maneno ya nguoni kupitia Instastories zao, huku Rayvanny naye vile vile akimjibu kwa maneno ya kashfa.

Wawili hao ambao wanaonekana kuridhi ugomvi wa Alikiba na Diamond, walitofautiana wazi mwaka 2021 baada ya sakata la bintiye KAJALA, Paula kudaiwa kutoka kimapenzi na Rayvanny, ambapo pia Harmonize alisemekena kumtongoza kwa kumtumia picha za utupu wake wakati bado anatoka kimapenzi na mama yake, Fridah Kajala.