"Naweza kutulia na nyoka 100 chumbani!" Diamond ajigamba huku akifichua tatizo analoishi nalo

Diamond alifichua kwamba anaogopa urefu kuliko kitu chochote maishani.

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo  alipiga kifua kwamba anaweza kuwa kwenye chumba kimoja na hata nyoka mia bila woga.

•Bosi huyo wa WCB alidokeza kuwa kurekodi video ya tukio ambalo lilihitaji yeye kupanda juu ya jengo hakukuwa rahisi.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz amesisitiza kwamba hawaogopi nyoka.

Huku akionyesha picha za nyuma za video za muziki kwenye Instagram, mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 32 alipiga kifua kwamba anaweza kuwa kwenye chumba kimoja na nyoka mia bila woga.

Diamond badala yake alifichua kwamba anaogopa urefu kuliko kitu chochote maishani.

"Hata kuwa juu ya meza kwangu inahisi kama kujitoa uhai kwa sababu ya akrofobia (hofu mbaya ya urefu mkubwa)," alisema.

Bosi huyo wa WCB alidokeza kuwa kurekodi video ya tukio ambalo lilihitaji yeye kupanda juu ya jengo hakukuwa rahisi.

Msanii wake, Mbosso Khan alionekana kumtia moyo na kumtaka asiwe na hofu ya urefu hata usio mkubwa sana.

"SIMBA hapandagi pandani wewe,hebu tufuatilie Mbugani utajua.. sie watu wa kuwinda kwa chini, lazima niheshimu mila," alisema.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya mwanamuziki huyo kufichua kwamba amejipatia nyoka wa kumuondolea upweke nyumbani.

Katika tangazo lake siku ya Ijumaa, Diamond alibainisha kuwa siku zote kumiliki nyoka kipenzi imekuwa ndoto yake.

Staa huyo wa Bongo mwenye umri wa miaka 32 alimtambulisha nyoka huyo wake kama rafiki yake mpya.

"Siku zote nimekuwa na shauku ya kuwa na nyoka wangu kama kipenzi ❤️🐍.. jameni kukutaneni na rafiki yangu mpya," alitangaza.

Aliambatanisha ujumbe huo na video yake akicheza na mnyama huyo anayeteleza huku kundi kubwa la watu wakiwa wamemzunguka.

Katika video hiyo, alisikika akikiri upendo wake mkubwa kwa nyoka na kueleza furaha yake kwa kumpata wa kufuga nyumbani

"Huyu mimi namfuga mnyama huyu nyumbani. Mimi napenda nyoka sana," alisika akisema.

Umati ulitazama kwa udadisi alipokuwa akichezea na nyoka huyo kwa usaidizi wa mwanamke aliyekuwa akimuonyesha jinsi ya kumshika. Hakuonesha uoga wowote na badala yake alionekana kufurahi sana kumshika.

Mwimbaji huyo anayetambuliwa kote duniani alifichua kwamba nyoka huyo wake atatambuliwa kwa jina  Chichi.