"Mwanamke bila kitambi labda hupendwi ama haushibi" - Omanga awatania wanawake

Maoni hayo yalipokelewa kwa njia mseto na wafuasi wake, baadhi wakisema alikuwa anatafuta njia ya kutetea ukubwa wa tumbo lake.

Muhtasari

• Wengine walisema kuwa kuwa na tumbo kubwa ni dalili ya matatizo ya afya na madhara yake ni mengi.

Millicent Oamnga kuhusu suala la kitambi kwa wanawake
Millicent Oamnga kuhusu suala la kitambi kwa wanawake
Image: Facebook

Aliyekuwa seneta maalum Millicent Omanga amezua maoni kinzani kwenye mtandao wa Facebook baada ya kuibua mjadala wenye utata kuhusu wanawake wenye vitambi au tumbo kubwa na wale wasio na tumbo kubwa bila mimba.

Omanga alipakia rundo la picha kwenye ukurasa wake akiwa na vikundi vya wanawake wengine katika maeneo ambayo hakusema ni wapi, wote wakiwa wamevalia nguo ndefu za kuonesha maeneo yao ya tumbo.

Hapo ndipo alitoa kauli kwamba mwanamke kamili ni yule ambaye ana tumbo kubwa linaloonekana wazi.

Kulingana na Omanga, mwanamke yeyote bila tumbo kubwa labda kuna mawili yanayomsibu – ama hapendwi au hashibi wakati anakula ndio sababu ya kutoonekana kwa tumbo lake.

Mwanamke bila kitambi labda hupendwi ama haushibi,” Millicent Omanga aliandika kwa utani akimalizia na emoji ya kuaibika akifunika uso.

Baadhi walihisi alikuwa anazua utani tu kuhusu picha hizo walikoonekana na wanawake wengine akiwemo yeye mwenyewe na kitambi lakini kuna wengine walilivalia njuga suala hilo kwa kumkosoa na kukanusha kauli yake vikali.

Wengine walimkumbusha kuwa kitambi ni ishara au dalili kwamba unafanya vibaya sana katika sekta ya afya ya mwili na tiba yake ni kushiriki mazoezi ili kuua kabisa tumbo kubwa.

“Umekosea Madame Bosi. Kitambi ni rundo la maswala ya kiafya... shinikizo la damu, ufuta mwingi mwilini, fetma, kisukari n.k..” Mike K Boit alimrudisha kwenye darasa la afya.