Msanii DNA: Nilipelekwa 'rehab' mara tatu, ulevi uliniathiri sana

DNA alifichua kwamba kwa wakati mmoja, alitumbuiza uwanja uliojaa watu elfu 40 nchini Tanzania.

Muhtasari

• Katika podcast moja, DNA alifunguka jinsi ulevi ulimuathiri na nusra kudidimiza nyota yake ya muziki, na jinsi alijikusanya baada ya kuporomoka.

Msanii DNA.
Msanii DNA.
Image: Screengrab.

Msanii Dennis Kagia Waweru, ambaye wengi wanamjua kama DNA, shukrani kwa vibao moto alivyovipakua miaka kadhaa iliyopita, kwa mara ya kwanza amezungumzia jinsi maisha ya ustaa yalimuathiri kipindi anapeperuka kwenye angaa za juu Zaidi kimuziki.

Katika podcast moja, DNA alifunguka jinsi ulevi ulimuathiri na nusra kudidimiza nyota yake ya muziki, na jinsi alijikusanya baada ya kuporomoka.

Kagia alisema wazi kuwa katika maisha yake, alijikuta katika vituo vya kurekebisha tabia kwa kimoto ‘rehabilitation centre’ mara tatu ambapo waliokuwa wanampenda walimpeleka huko ili kujaribu kumnusuru kutokana na ulevi.

“Nilikuwa na mwanzo mya mgumu sana katika maisha yangu. Naweza sema nilianza maisjha upya baada ya kugundua kwamba vitu vingi nilivyokuwa navifanya havikuwa vinaleta tija katika maisha yangu. Tulikuwa tunaamka asubuhi manze tumegonga vilevi, pengine naamka saa tano naona nimetafutwa kwa simu kadhaa kutoka kwa produsa ndio akili zinapiga kwamba, ninaharibu.”

“Kusema kweli nimekuwa katika kituo cha kurekebisha tabia mara tatu. Si hadithi ya kuhuzunisha kwangu na sioni kama kuna kunyanyapaliwa kwa njia yoyote upande wangu. Ninaizungumzia kwa sababu ninahisi watu wanateseka kutokana na matatizo ambayo yanaweza kutatuliwa,” DNA alisimulia.

Msanii huyo aliyetamba na vibao kama ‘Banjuka Tu’, ‘Maswali Mengi’ na vingine alifunguka kwamba kando na kuimba, wengi hawajui kuwa alikuwa kuwa mzalishaji wa midundo ya miziki, mbunifu wa majukwaa ya kusambaza kazi za wasanii na mambo mengine mengi ambayo aliyafanya kipindi kile ambacho dijitali haikuwa imebisha hodi.

“Wakati nilianza kuzalisha miziki, msanii wa kwanza nilitoa alikuwa Chris Kantai marehemu na nilitoa wengine wengi ambao nilisaidia kuandika miziki,” DNA alisema. “Pia mimi ndio nilizalisha Fimbo Chapa nilipoenda lebo ya Grandpa, pamoja na Kidis na wengine. Popote unaniona, kuna matunda mazuri.”

Msanii huyo alisema ugumu wa kupata pesa enzi wanaimba uliwataabisha sana. Alisema iliwabidi waungane na wasanii wengine kama Jaguar, Juliani, Juacali ili kuweka miziki yao pamoja na kuiweka kwa CD na kuanza kuzisambaza katika mtaa wa River Road, jijini Nairobi.

DNA alifunguka kwamba kwa wakati mmoja alikuwa anasafiri kutoka Nairobi kwenda Dar es Salaam kwa basi kutwa nzima kwa ajili ya kusambaza miziki yao ambayo ilikuwa inafanya vizuri huko.