Ramadhani ikiisha tunaanzia tulipoishia - Simba wa WCB Wasafi anguruma

Mapema mwaka ukianza, Diamond aliahidi kuwa mwaka huu ni wimbo baada ya wimbo, akidokeza kuimba hadi kwa Kichina.

Muhtasari

• Diamond sasa anasema kuwa baada ya Ramadhani, mwendo ule ule utarejelewa na kuwataka mashabiki kukaza buti.

Diamond Platnumz asema baada ya ramadhani mwendo ni ule ule, ngoma baada ya ngoma.
Diamond Platnumz asema baada ya ramadhani mwendo ni ule ule, ngoma baada ya ngoma.
Image: Instagram

Msanii namba moja wa muda wote katika miziki ya kizazi kipya ya Bongo Fleva ukanda wa Afrika Mashariki, Diamond Platnumz amejibu ni kwa nini amekuwa mkimya kwa siku za hivi karibuni licha ya mwanzoni mwa mwaka kuahidi mashabiki wake kuwa angeachia nyimbo baada ya nyimbo.

Akijibu hilo, msanii huyo ametoa ahadi kwa mashabiki wake kuwa amewaandalia mambo makubwa, mazito na mazuri punde tu mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani utakapomalizika.

Platnumz alisema kuwa yupo kwenye mfungo wa Ramadhani na kusema pindi atakaporudi, mwendo ni ule ule wa kuachia kibao baada ya kingine kwa mfululizo ambao aliuita “nunda juu ya chuma”.

Msanii huyo alipakia video kwenye Instastory yake akishiriki mazoezi ya kuimba na watu wengine na kusema kwamba ni maandalizi ya pindi baada ya kumaliza kufunga wiki mbili na nusu zijazo.

“Kwa kifupi ni kwamba Ramadhani ikiisha tu, tutaanzia tulipoishia,” Simba wa WCB Wasafi alinguruma.

Miongoni mwa walioonekana naye kwenye studio ni mtayarishaji wa midundo S2Kizzy na ndugu zake na kwa muonekano wote walikuwa wanatayarisha dude ambalo huenda mashabiki wa Diamond wakapakuliwa pindi baada ya mwezi wa Ramadhani kukamilika.

Mapema mwaka ukianza, Diamond aliwahakikishia mashabiki wake kwamba ni wakaati wa kutoa miziki kwa mwendelezo hadi pale watajihisi fahari na kujivunia kuwa naye kama msanii wao.

Hata hivyo, alitoa taadhari kwao kwamba katika mwendelezo wa ngoma zake, wasije wakashangaa endapo watamsikia akiimba lugha zingine za kigeni wasizozielewa ikiwemo Kichina.

Kwa kuwaaminisha mashabiki katika maneno yake, msanii huyo alianza kwa kasi ya duma kwa kuachia vibao 3 moto chini ya wiki mbili, Yatapita, Zuwena na My Baby, vibao ambavyo vimekuwa vikifanya vizuri na kulirudisha jina lake kwenye chati za muziki kabla ya kwenda kimya tena ghafla, haswa mwezi wa Machi msanii huyo hajasikika kama alivyoahidi.