Bensoul afunguka kuhusu kuondoka Sol Generation

Bensol alisema kwamba mkataba wake katika kundi hilo uko karibu kuisha.

Muhtasari

•Katika mahojiano na Tuko Extra, Bensol alisema kwamba mkataba wake katika kundi hilo uko karibu kuisha.

Image: hisani

Mwimbaji  Benson Mutua almaarufu Bensoul ametangaza kuwa anatarajia kuondoka kwenye bendi ya Sauti Sol hivi karibuni.

Katika mahojiano na Tuko Extra, Bensol alisema kwamba mkataba wake katika kundi hilo uko karibu kuisha.

Alifanananisha kuondoka kwake na simbajike anayewalea watoto wake kisha kuwaachilia kwenda kujitafutia pindi wanapokuwa wakubwa na wenye uwezo wa kujikimu akisema kuna wanasimba watakaoweza kujikimu na kubakia hai ilhali wengine watakufa.

"Mimi ni kama dume simba wa jangwani, wakifika miaka fulani ,huwa wanafukuzwa kutoka kwenye kundi ili wajitafutie, kawaida hutimuliwa wakiwa wengi hivyo basi wengine wataweza  kujikimu ilhali wengine wataangamia jangwani," alisema Bensoul.

Aliongezea kuwa amejijenga na kazi yake yake muziki.

"Ni jambo zuri sana, tumekuwa na wao, na tumejenga himaya sote," alikiri.

Bensol alijiunga na Sauti Sol mwaka wa 2019 baada ya lebo ya Sol Generation kufunguliwa rasmi.

Bensoul ni mwanamuziki wa Kenya mwenye umri wa miaka 27. Aliingia kwenye sanaa ya muziki akiwa eneo alikozaliwa la Embu.Amekuwa kwenye sanaa hii kwa karibu miaka 10 sasa. Wakati mmoja, Bensol alisema kuwa hafuati kujulikana ila kuwacha msingi bora na kuleta utofauti katika kazi ya muziki.

Bensoul ni mchezaji wa gitaa na  piano. Alifichua kuwa alipokuwa mdogo, babake alikuwa anacheza gitaa kanisani ilhali mamake alikuwa anaimba kwenye kwaya ya kanisa.

Bensoul amewaandikia nyimbo baadhi ya mastaa na mabendi kama vile H_ Art The Band, Sauti Sol, Mercy Masika na wengineo.

Baadhi ya vibao vyake ni kama vile Medicine, Forget you, Not Ready , Pombe Sigara kati ya nyinginezo.