Iphone ya mpenzi wa Aslay yalipuka na kuchoma godoro wakiwa wamelala

Mrembo huyo kwa jina Tessy Chocolate alisema simu hiyo ilikuwa imechomekwa kwenye chaji wakati ililipuka ghafla na kushika moto.

Muhtasari

• "Kumelipuka tumechanganyikiwa, ilikuwa kwenye chaji na huu ni mto,” Tessy Chocolate alisema akionesha madhara ya simu hiyo kwenye mto.

• Mrembo huyo aliwataka watu kuwa makini na kuweka simu kwenye chaji kisha kuziweka pembeni wakiwa wamelala.

Tessy Chocolate asimulia jinsi simu yake ilivyolipuka ikiwa kwenye chaji.
Tessy Chocolate asimulia jinsi simu yake ilivyolipuka ikiwa kwenye chaji.
Image: Instagram

Mrembo Tessy Chocolate, ambaye ni mzazi mwenza wa msanii Aslay Isihaka  amesimulia kitendo cha ajabu ambacho kilimtokea baada ya simu yake aina ya Iphone kulipuka na kuchomeka ikiwa kwenye chaji.

Tessy alipakia video ya simu hiyo ikiwa imeungua kabisa lakini pia ikiwa imeunguza hadi mto wa kitanda alilokuwa ameiweka juu ikiendelea kupata chaji.

“Jamani tusilale na simu ikiwa kwenye chaji. Hili limenitokea leo, simu ilikuwa kwenye chaji, imelipuka na kuwaka. Kumelipuka tumechanganyikiwa, ilikuwa kwenye chaji na huu ni mto,” Tessy Chocolate alisema akionesha madhara ya simu hiyo iliyokuwa imeungua kabisa pamoja na kuunguza mto.

Tessy ambaye walitengana na Aslay alisema kuwa tukio hilo lilitokea mwendo wa alfajiri ambapo alikuwa amelala kitandani na ndugu yake na pembeni mwake kulikuwa na simu yake ya Iphone ambayo ilikuwa imechomekwa kwenye chaji.

“Tulikuwa tumelala saa kumi na mbili asubuhi, na ndugu yangu. Yeye ndiye alikuwa amelala huo upande ambapo simu ililipuka, ni simu yake. Kilichotokea ni mlipuko halafu moto ukawa unatoka kama ule wa kupuliza. Ni kitu cha sekunde kama 30 hivi, kilitokea kwa haraka mno,” Tessy alisema.

Mrembo huyo aliwataka watu kuwa makini na kuweka simu kwenye chaji kisha kuziweka pembeni wakiwa wamelala kwani madhara ambayo yanaweza kusababishwa na mlipuko wao ni makubwa kupita maelezo.

Tessy alisema kuwa walikuwa na bahati kwani mlipuko huo ulitokea alfajiri wakiwa angalau usinginzi umeisha, na kusema ingekuwa ni usiku wa manane wakati wa usingizi wa pono basi mengine yangewapata.

Kulingana na wataalam wa kisayansi kuhusu vifaa vya kielekroniki, haifai kuweka vifaa vya kielektroniki katika mto au pembeni mwako kitandani ukiwa umelala navyo vikiwa vimechomekwa kwenye chaji kwani vinaweza vikachukua moto Zaidi na kulipuka.

“Usichaji kifaa chochote cha umeme, ikiwa ni pamoja na simu na kompyuta kibao, kwenye kitanda chako au chini ya mto wako unapolala kwani zinaweza kupata joto kupita kiasi na kusababisha moto. Ikiwezekana, epuka kuchaji vifaa bila mtu kutunzwa au usiku kucha, na inapohitajika tu vichaji kwenye sehemu ngumu kama vile dawati,” Electrical Safety First wanashauri.