Diamond amlipua Harmonize bila huruma, "Range Rover ni magari ya watoto wa kike tu!"

Diamond alionekana kumjibu Harmonize kwa kauli kuwa msanii bila gari la Range hafai kumuongelesha wala kuweka kwenye orodha ya wasanii 'serious'.

Muhtasari

• "Naomba kuanzia leo niweke rasmi kwamba magari ya Range Rover ni maalum kwa ajili ya malkia ambao ni wapambanaji mjini" - Diamond.

Diamond amjibu Harmonize kuhusu wasanii kumiliki range rover.
Diamond amjibu Harmonize kuhusu wasanii kumiliki range rover.
Image: Instagram

Wiki moja baada ya Harmonize kuwakejeli wasanii wa Afrika Mashariki ambao hawamiliki magari aina ya Range Rover, mbaya wake katika muziki Diamond Platnumz amemjibu vikali akisema kuwa gari aina ya Range Rover ni la kutumiwa na watoto wa kike tu.

Harmonize katika taarifa yake ya shobo, alisema kuwa msanii yeyote ambaye anajua hana gari la Range Rover asimuongeleshe wakikutana na wala hafai kuwekwa katika orodha ya wasanii ambao wako ‘serious’ na kazi zao za muziki.

Sasa Ijumaa baada ya Zuchu kudai kujinunulia Range Rover jipya, watu mbalimbali walimhongera akiwemo bosi wake Diamond Platnumz.

Katika ujumbe wake wa kumhongera Zuchu ambaye pia za ndani zinadai ni mpenzi wake, Diamond alionekana kumfuma vikali Harmonize akisema kuwa magari ya Range ni ya watoto wa kike tu ambao wanajibidiisha kimaisha.

Aidha, msanii huyo alisema kuwa Zuchu anampa fahari kubwa sana kuona kuwa ameweza kumlea msanii ambaye anafikia hatua ya kumiliki mali ghali kiasi hicho.

“Unanifanya nitembee kifua mbele Zuuh, naomba kuanzia leo niweke rasmi kwamba magari ya Range Rover ni maalum kwa ajili ya malkia ambao ni wapambanaji mjini, wakiongozwa na wewe Zuchu,” Diamond alisema.

Baadhi walihisi kwamba ujumbe huu wa kusema rasmi magari ya Range ni ya watoto wa kike ulikuwa unatupa taarifa ya bomu la moto kule Konde Village, kumsuta Harmonize kwa kudai kuwa magari hayo kwake ni kama wapenzi wake tu, kwani hawezi kuisha bila.

Itakumbukwa pia mapema wiki hii Radio Jambo iliripoti kuwa msanii Nandy aliweza kumnunulia mpenzi wake Billnass gari jipya aina ya Range Rover kama zawadi ya siku yake ya kuzaliwa.

Baadhi ya wasanii na watu maarufu kutoka Bongo ambao hivi karibuni wametangaza kumiliki magari aina ya Range Rover ni Esma Platnumz, dadake Diamond, Sishkiki Sikamatiki, mjasiriamali wa nguo ambaye alisema alituzwa gari hilo na mtu ambaye hakumtaja – japo za chini ya zulia zilidai kuwa ni Harmonize, na wengine wengi bila kumsahau Kajala Masanja.