Kwa nini Marioo hakusainiwa na Diamond kuziba pengo la Rayvanny? Meneja afunguka makubwa!

"Hatuamini kwenye ili mtu akue ni lazima akanyage kichwa cha mtu, hatuamini kabisa. " - Meneja alisema.

Muhtasari

• "Mimi nilitumia nguvu yangu, nimeongea na Babu Tale sana, bwana hakuna mtu aliyekuwa anataka kitu kama hiki" - Meneja alisema.

Meneja wa Marioo azungumza kwa nini hakusainiwa na Diamond.
Meneja wa Marioo azungumza kwa nini hakusainiwa na Diamond.
Image: Instagram//Marioo

Kwa mara ya kwanza kabisa tangu sekeseke za Marioo kuomba kusainiwa na Diamond katika lebo ya WCB Wasafi kuibuka, meneja na produsa wa msanii huyo amefunguka kilichokwamisha usajiri huo.

Akizungumza katika kipindi cha TheSwitch ndani ya kituo cha Wasafi, meneja ambaye pia ni mzalishaji wa nyimbo Abbah alisema kuwa jambo la Marioo kutaka kusainiwa na Diamond kuziba pengo la Rayvanny aliyeondoka zake Next Level Music ni kitu ambacho hawakuwa wanataka kitokee kama menejimenti.

Abbah alisema kuwa sakata hilo lilipotokea kama miezi miwili hivi iliyopita, walihaha sana kulituliza, ikiwemo kumtaka Marioo kukoma kulijadili mitandaoni na pia wao kuzungumza na uongozi wa Diamond kuhusu hilo.

“Kwanza kabisa tulinyamaza kabisa, kutowajibu watu. Mimi naamini kwenye ambavyo naamini, Diamond ni jamaa muungwana sana na sidhani kama Marioo kulizungumza kivingine lilimkera. Mimi nilitumia nguvu yangu, nimeongea na Babu Tale sana, bwana hakuna mtu aliyekuwa anataka kitu kama hiki, kama kimetokea na picha imekuwa hivi, hatukuwa tunataka iwe hivyo kabisa,” Abbah alisema.

Abbah pia alisema kuwa katika uongozi wake, anaamini sana katika mtu kufanikiwa kwa bidii yake na wala si kubebwa kwenye mabega na mtu Fulani mwenye ushawishi ili kutusua kimuziki.

“Sio kitu ambacho tunakiamini kwenye uhangaikaji wetu kabisa. Hatuamini kwenye ili mtu akue ni lazima akanyage kichwa cha mtu, hatuamini kabisa. Sisi huwa tunafanya kadri ya uwezo wetu ili twende na vitu vyetu,” Abbah alibainisha.

Baada ya taarifa hizo kudai kuwa Marioo aliomba kusainiwa Wasafi, msanii huyo mwenyewe alijitokeza na kukanusha, akisema kuwa Diamond huenda alijichanganya.