Bahati tumbojoto kuhusu kazi mpya ya mkewe Diana kwenye kipindi cha kuchumbiana runingani

Hata hivyo, Dr Ofweneke alimhakikishia Bahati kuwa mke wake atakuwa kwenye mikono salama na kuahidi kumrudisha kwake baada ya vipindi 14.

Muhtasari

• Kipindi hicho kitakuwa kinaongozwa na mchekeshaji Dr Ofweneke na msanii Diana Marua.

• Baada ya Bahati kuonesha wasiwasi wake, Dr Ofweneke alimhakikishia kuwa mke wake atakuwa kwenye mikono salama.

Bahati aingiwa tumbojoto kuhusu kazi mpya ya Diana Marua.
Bahati aingiwa tumbojoto kuhusu kazi mpya ya Diana Marua.
Image: Instagram

Wikendi iliyopita, Startimes walikuwa wanazindua msimu wa tatu wa mwendelezo wa kipindi cha uhalisia cha kuchumbiana runingani cha Hello Mr Right.

Kipindi hicho kitakuwa kinaongozwa na mchekeshaji Dr Ofweneke na msanii Diana Marua.

Katika uzinduzi wa kipindi hicho cha kuchumbiana, mumewe Diana Marua, Bahati Kioko alionesha wasiwasi wake kuhusu kazi hiyo mpya ya mkewe, akionekana kuingiwa na mashaka kuwa huenda mengine yakatokea katika mazungumzo kuhusu suala zima la kuchumbiana.

“Tafadhai, mimi sijakuja kukusapoti, hata sijakuja kuona uzinduzi, nimekuja tu kuona vile unakaribiana na mke wangu. Huko kukaribiana chunga sana eeh,” Bahati alimwambia Dr Ofweneke.

Lakini kwa hali ya ucheshi, Dr Ofweneke alimjibu kwamba sifa zake zinajulikana ila akamhakikishia Bahati kuwa mke wake atakuwa kwenye mikono salama.

“Kaka sifa zangu zinajulikana. Mimi ni mwanamume mzima katika kila kitu. Lakini naweza kukuahidi kama kaka yangu mdogo mke wako yuko kwenye mikono salama. Baada ya vipindi 14 nitamrudisha akiwa salama na mzima. Shukrani sana kwa kumkubalia kuja katika kipindi hiki, nitamlinda,” Dr Ofweneke alimhakikishi Bahati.

Baada ya hafla ya uzinduzi rasmi, Bahati alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii na kummwagia sifa Diana, akisema anajivunia mafanikio yake na anampigia saluti kwa kuwa na bidii na bidii kila wakati.

“Tena niseme mimi ni Mume wa Fahari. Mpenzi wangu, kila siku Unanifanya Nijivunie. Tulianzisha Chapa hii ya #DIANA_B hivi majuzi tu na sasa Jitazame… Ninaweza kukuita kwa Ujasiri Mtayarishaji wa Maudhui Anayependwa na Kila Mtu!” Bahati aliandika.

Diana alionyesha kufurahishwa kwake na jukumu hilo jipya na kuahidi kujitolea kwa uwezo wake wote ili kuhakikisha kuwa onyesho hilo linaburudisha na kuelimisha.

Dr Ofweneke ambaye amekuwa sehemu ya shoo hiyo tangu msimu wa kwanza, alionyesha kufurahishwa na mafanikio ya vipindi vilivyopita na kuahidi kutoa bora zaidi.