Diana B: Mume wangu Bahati alininunulia marashi ya elfu 62 Dubai

Bahati alisema kwamba Diana alikuwa anataka kununuliwa saa ya elfu 24.

Muhtasari

• "Alikuwa amelala lakini nilimuamsha na nikamuambia nataka hii, marashi yenye thamani ya elfu 62" - Marua.

Bahati amnunulia Diana Marashi ya 62k
Bahati amnunulia Diana Marashi ya 62k
Image: Instagram

Baada ya takribani siku kumi wakifanya ziara jijini Dubai, wanandoa Bahati Kioko na Diana Marua walirejea Kenya kwa mbwembwe kuu siku mbili zilizopita.

Wapenzi hao walikwenda Dubai kujivinjari ambapo pia waliangukia dili la kuteuliwa kama mabalozi wa utalii wa Dubai wakiwakilisha ukanda wa Afrika Mashariki na kati.

Diana Marua sasa amefichua kwamba mumewe Bahati alimnunulia marashi ghali ya shilingi elfu 62 jijini Dubai na kuwataka mashabiki wote ambao watapata nafasi ya kukutana naye kuhakikisha kwamba wanahisi harufi nzuri ya marashi hayo ghali.

“Marashi haya alininunulia kwa ndege, elfu 62 nilimuambia mpenzi wangu nataka hii. Unajua aliniambia nini, angalia katika kitabu hicho na uchague unachokitaka baada ya kufanya uamuzi wako. Alikuwa amelala lakini nilimuamsha na nikamuambia nataka hii, marashi yenye thamani ya elfu 62 marafiki zangu! Kama utakutana na mimi hakikisha unaninusa,” Diana Marua alisema.

Wapenzi hao pia walipakia video na picha wakila bata nono kule jangwani wakiwa wamevalia vilemba kama Waarabu halisia.

Awali Bahati alidokeza kwamba mke wake Diana Marua alikuwa amemsihi kumnunulia jumba la kujistarehesha huko Dubai ili awe akienda kule mara kwa mara kujiburudisha.