Binti wa CR7, pacha aliyesalimika baada ya kifo cha pacha mwenza afikisha mwaka mmoja

Katika mahojiano, Ronaldo alifichua kwamba aliweka majivu ya pacha aloyefariki kwenye kona ya kanisa nyumbani kwake na huyaombea pumziko la amani kila wakati.

Muhtasari

• “Heri ya mwaka wa kwanza wa maisha mpenzi wangu. Baba anakupenda sana!” Ronaldo aliandika.

• Rodriguez na supastaa wa Al Nassr Ronaldo walipata mtoto wao wa kwanza pamoja, Alana Martina, mwaka wa 2017.

CR7 amsherehekea binti yake Bella Esmeralda kufikisha mwaka mmoja.
CR7 amsherehekea binti yake Bella Esmeralda kufikisha mwaka mmoja.
Image: Instagram

Mchezaji nambari moja duniani Mreno Christiano Ronaldo anasherehekea binti yake Bella Esmeralda kufikisha mwaka mmoja tangu kuzaliwa wakiwa mapacha.

Mnamo Aprili 18 mwaka 2022, mpenzi wa Ronaldo, Georgina Rodriguez alijifungua mapacha – wa kike na kiume, lakini kwa bahati mbaya yule wa kiume alifariki huku wa kike akisalimika. Walimpa jina Bella Esmeralda.

Ronaldo alipakia picha kwenye mitandao yake ya kijamii akiwa amempakata binti huyo wake Aprili 18, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuzaliwa na kumwandikia ujumbe mtamu katika miezi 12 ya maisha yake.

“Heri ya mwaka wa kwanza wa maisha mpenzi wangu. Baba anakupenda sana!” Ronaldo aliandika ujumbe wa hakikisho la mapenzi ya baba kwa bintiye.

Rodriguez na supastaa wa Al Nassr Ronaldo walipata mtoto wao wa kwanza pamoja, Alana Martina, mwaka wa 2017 kabla ya kuzaliwa kwa binti Bella Esmeralda Aprili mwaka jana.

Mwanamitindo huyo wa Uhispania na mwanasoka wa ureno walitarajiwa kupata mapacha, lakini Bella pekee ndiye aliyenusurika wakati wa kujifungua huku kaka pacha Angel akifariki dunia kwa huzuni.

Ronaldo, ambaye alikuwa na wana Cristiano Jr na Mateo na binti Eva Maria kabla ya uhusiano wake na Rodriguez, alifichua kuwa aliweka majivu ya mtoto wake kwenye kanisa nyumbani kwake.

Akizungumzia mimba zake za awali, Rodriguez alisema: “Kila nilipokuwa nikienda kwa madaktari wa magonjwa ya wanawake usiku, nilikuwa nikiota ndoto za kutisha kwa sababu nilikuwa na wasiwasi kuhusu watakuwa kwenye nafasi gani, uzazi ungekuwaje, ikiwa ni upasuaji.

 

"Niliogopa sana kila vipimo vya ultrasound. Nilihisi mkazo sana kwa sababu nilikuwa na mimba tatu za awali na nilirudi nyumbani vipande-vipande.”

Mpenzi wa Ronaldo alifichua kwamba "kipande cha moyo wangu kilipasuka" baada ya Angel kufariki na hapo awali ilikuwa vigumu kuwaambia watoto wake kilichotokea.