Diamond amtema Aliko Dangote na kujiita Sheikh Mansour, tajiri wa Manchester City

Mansour ni mmoja wa familia ya kitajiri ya Abu Dhabi ambao ndio wanaongoza na kumiliki asilimia kubwa ya utajiri wa taifa la Miliki za Kiarabu, UAE.

Muhtasari

• Kando na kumili utajiri wa UAE, Mansour pia ni mmiliki wa klabu ya Manchester City nchini Uingereza.

Diamond Platnumz alitupa jina la Dangote, ajiita Sheikh Mansour.
Diamond Platnumz alitupa jina la Dangote, ajiita Sheikh Mansour.
Image: Instagram

Msanii Diamond Platnumz amehisi kukua Zaidi kibiashara na katika utajiri na hivyo kulitema jina la tajiri namba moja Afrika Aliko Dangote na badala yake sasa ameanza kujiita jina la bilionea tajiri kutoka miliki za Kiarabu, Sheikh Mansour.

Msanii huyo tajiri Zaidi kutoka nchini Tanzania alijibatiza jina la kimajazi la Aliko Dangote takribani miaka 10 iliyopita, kama njia moja ya kujitambulisha kama tajiri wa muziki ukanda wa Afrika Masahriki.

Dangote kwa Zaidi ya miaka 10 amekuwa akiibuka kidedea katika orodha ya matajiri Afrika, kwa mujibu kwa jarida la Forbes.

Diamond kwa kufuata nyayo zake, aliazimia kujiimarisha katika mduara wa ukwasi na akajipa jina la Dangote baada ya kuanzisha lebo yake ya Wasafi ambapo baadae alifungua kituo cha runginga cha Wasafi TV na kisha redio ya Wasafi FM.

Lakini kadri ambavyo amezidi kukua kibiashara mpaka kuanzisha kampuni ya Kamari ya Wasafi Bet miongoni mwa biashara zingine, Diamond ni kama ameona viwango vya Dangote tena havimshawishi na badala yake ametanua mbawa zake nje na kwenye viwango vya juu Zaidi ambapo anaona Sheikh Mansour ndiye himizo la kishua.

Baada ya kufanikiwa kukibooa kipindi cha asubuhi katika kituo cha redio cha EFM kwa kuwanyakua watangazaji wawili na kuwarudisha Wasafi, msanii huyo aliwalaki kwa msafara wake na baadae akapakia picha yake akiwa amevalia joho la Kiislamu akijiita Sheikh Mansour.

Sheikh Mansour ni mmoja wa wanafamilia tajiri Zaidi kutoka Abu Dhabi ambaye pia anamiliki kampuni mbalimbali ikiwemo ile ya kimichezo inayomiliki timu ya kandanda kutoka Uingereza ya Manchester City.

Anajihusisha na makampuni mbalimbali yanayoendeshwa na serikali katika UAE. Yeye ni mwenyekiti wa Baraza la Maendeleo la Mawaziri, Mamlaka ya Uwekezaji ya Emirates na Mamlaka ya Mashindano ya Emirates.

Anaketi katika Baraza Kuu la Petroli na Baraza Kuu la Masuala ya Kifedha na Kiuchumi. Mansour ni mwanachama wa bodi za Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Abu Dhabi na Mamlaka ya Uwekezaji ya Abu Dhabi (ADIA).

Yeye pia ni makamu mwenyekiti wa Kampuni ya Uwekezaji ya Mubadala, hazina ya utajiri wa serikali ya Emirati na pia ni mwenyekiti wa benki kuu ya UAE.