Wema Sepetu azungumzia rushwa ya ngono kuelekea ushindi wake wa 'Miss Tanzania 2006'

Sepetu alisema kuwa mpaka anashinda tuzo ya Miss Tanzania mwaka 2006, alikyuwa bikira.

Muhtasari

• Mrembo huyo alisema kuwa aliwahi kuzisikia tuhuma hizo za rushwa ya ngono lakini hakuwahi kushiriki wala kushuhudia.

Wema Sepetu azungumzia rushwa ya ngono kuelekea ushindi wake wa miss Tanzania
Wema Sepetu azungumzia rushwa ya ngono kuelekea ushindi wake wa miss Tanzania
Image: Instagram, Matkaba

Msanii wa muda mrefu kutoka Tanzania, Wema Sepetu amefunguka kuwa licha ya kwamba kuna dhana kuwa ili mtu, haswa mtoto wa kike kupata kitu na upendeleo ili kukwea hadi kwa umaarufu, ni sharti atoe rushwa ya ngono, yeye hajawahi shiriki katika vitendo hivyo vichafu.

Katika mahojiano ya kipekee na chaneli ya Manara TV, Sepetu alisema kuwa wengi huenda wanaamini kuwa kushinda kwake tuzo ya Miss Tanzania mwaka 2006 kulitokana na yeye kutoa rushwa ya ngono, jambo ambalo alilifutilia mbali na kusema kuwa hakuwahi jipata katika mkondo huo.

“Hizo tuhuma za kutoa rushwa ya ngono nimeshawahi zisikia lakini sijawahi shiriki. Ukweli mmoja ambao nitausema ni kwamba sijawahi toa rushwa ya ngono. Mimi mpaka nashinda Miss Tanzania nilikuwa bikira,” Sepetu alisema.

Mpenzi huyo wa Whozu alisema kuwa licha ya kwamba alianzia katika urembo na kumpelekea kushinda tuzo ya Miss Tanzania mwaka 2006, lakini kitu kikubwa ambacho anakipenda na muda wote atakumbuka ni kuwa mbele ya kamera akiigiza filamu.

“Nisiseme uongo mimi nafurahia sana nikiwa mbele ya kamera naigiza. Nafurahia sana kwa sababu yaani naipenda sana ile kazi ya kuigiza. Mimi nimeanzia katika tasnia ya urembo lakini nimeonekana Zaidi nilivyoingia kwenye tasnia ya filamu. Kuwa Miss Tanzania kilikuwa kitu kimoja lakini pia kuwa mwigizaji kulikuwa kitu kingine kikubwa na tofauti kabisa,” Sepetu alisema.

Mrembo huyo alimmiminia sifa tele marehemu mwigizaji Steven Kanumba kwani ndiye aliyemtambua na kumuingiza kwenye filamu.

“Siku hiyo tumenda kutafuta fenicha na dadangu halafu tukapata watu wamejazana kumbe kulikuwepo na shoot inafanyika. Watu wake wakanikimbilia na kuniomba nipite japo kwa kuonekana tu kwenye shoot yao. Baada ya kumpa taji la Miss Tanzania mrembo mwingine, tukawa tunajuana na Kanumba kwa miezi mitano ndio akaniambia kuwa alikuwa anaona kitu ndani yangu,” Sepetu alikumbuka.

Mrembo huyo alisema kuwa kibarua chake cha kwanza na Kanumba ni kuigiza kama mlokole japo yeye kiasilia ni Muislamu katika filamu ya ‘Point of No Return’ ambapo alifana Zaidi ya matarajio ya wengi.