Je, Mbosso aliiga wazo la Video ya Bensoul 'Nairobi'?

Kuwiana kwa video ya Mbosso 'Amepotea' na Bensoul 'Nairobi' kunazua sintofahamu.

Muhtasari

• Mbosso, msanii mahiri aliyesajiliwa chini ya lebo ya Wasafi Records ya Tanzania, hivi karibuni alitoa video mpya ya wimbo wake unaoitwa "AmePotea."

• Hata hivyo, video hiyo imezua mjadala kutokana na kile kinachodaiwa kuwiana na video ya muziki iliyotolewa na msanii wa Kenya Bensoul.

Mbosso ambaye ni msanii mahiri aliyesajiliwa kwenye lebo ya Wasafi Records ya Tanzania, hivi karibuni alitoa video mpya ya wimbo wake unaoitwa "Amepotea."

Hata hivyo, video hiyo imezua mjadala kutokana na kile kinachodaiwa kuwiana na video ya muziki iliyotolewa na msanii wa Kenya Bensoul.

Katika video ya mbosso ya “AmePotea,” kuna matukio ambapo Mbosso anaonekana uchi kwenye beseni akiogeshwa na mwanadada anayedaiwa kumpenda.

Matukio haya yametajwa kuwiana na video ya Bensoul inayoitwa "Nairobi," ambapo pia anaonekana kwenye beseni akiogeshwa na mwanadada.

Mashabiki wengi wa Bensoul wameishutumu Wasafi Records kwa kuiba wazo lililoko kwenye video ya Bensoul, wakidai kuwa video ya Mbosso ni chapisho ya moja kwa moja ya "Nairobi."

Wanasema kuwa si sadfa matukio ya Mbosso kuogeshwa kwenye beseni kwa kuwa yanafanana sana.

Kwa upande mwingine, baadhi ya mashabiki wa Mbosso na Wasafi Records waliitetea video hiyo wakisema kuwa tukio hiyo ya kuogeshwa kwenye beseni si geni na kwamba video ya Mbosso ni ya kipekee kwa namna yake.

Wanasema kuwa matukio katika video ya Mbosso haijaigwa moja kwa moja kutoka  video ya Bensoul bali ni wazo la kawaida linalotumika katika video za muziki.

Mzozo huu unaangazia umuhimu wa uhalisia na ubunifu katika tasnia ya muziki.

Ingawa sio kawaida kwa wasanii kuazima wazo kutoka msanii mwenzake, ni muhimu kutoa sifa inapostahili na kuepuka kuiga moja kwa moja.

Utata uliohusu video ya “AmePotea” ya Mbosso na madai ya uwiano wa video ya Bensoul “Nairobi” unaibua maswali kuhusu maadili ya kukopa mawazo katika tasnia ya muziki.

Ni muhimu kwa wasanii na lebo za rekodi kudumisha uhalisia na ubunifu katika kazi zao, huku pia wakitoa sifa kwa wale ambao mawazo yao waliweza kuwa wameazima.