Kutana na ajuza wa miaka 123 ambaye ni bikira, bado hajakata tamaa ya kupata mume

“Kufikia muda nilikuwa na hisia za kutaka mume wa kunioa, nilikuwa tayari nimepita ujana wangu. Nilikuwa nimezeeka" - Ajuza alisimulia.

Muhtasari

• Licha ya umri wake kwenda, ajuza huyo alisema bado ana imani mume mzuri wa kumpenda na kumjali atatokea na kumuoa.

• "Ni kweli mimi ni bikira. Nilikuwa nafikiria sana kuhusu mapenzi kipindi niko mbichi" - ajuza.

Ajuza wa miaka 123 ambaye hajawahi kushiriki mapenzi hata mara moja.
Ajuza wa miaka 123 ambaye hajawahi kushiriki mapenzi hata mara moja.
Image: Screengrab//Afrimax

Ajuza mmoja mwenye umri wa miaka 123 amewashangaza wengi baada ya kuhadithia maisha yake ya taabu kuishi Zaidi ya karne moja bila kuwa na mume wala watoto.

Ajuza huyo kutoka kijiji kimoja nchini Rwanda aliiambia chaneli ya Afrimax kwamba katika maisha yake yote, hajawahi kupatana na mwanaume kimwili, achia mbali kuuona uchi wa mwanaume, na hivyo ameishi kama bikira.

“Katika maisha yangu yote, sijawahi kuwa na mwanamume, nina miaka 123. Hadithi yangu ni tofauti kidogo. Ni kweli mimi ni bikira. Nilikuwa nafikiria sana kuhusu mapenzi kipindi niko mbichi lakini sikuweza kukutana na mwanamume yeyote,” Ajuza huyo kwa jina Nyirakajumba Peragie alielezea kwa kusononeka.

Mkongwe huyo alisema kuwa ilianza mapema sana miaka ya 1900 alipobaleghe la katika mila za kijijini kwao, wasichana hawakuwa wanaruhusiwa hata kidogo kujumuika na wavulana.

Alisema kufuata tamaduni hiyo kumlifanya kujitenga kabisa na wanaume na kuishia kujipata anakaa mwenywe.

“Sikutaka kabisa kujumuika na wanaume. Nilikuwa nawaogopa sana wanaume na hilo pengine lilinizuia kutopata mpenzi katika maisha yangu yote ya ujana. Ningewaona wanaume wanakatiza misele nyumbani kwetu lakini sikuwahi kuwa na hisia kwao,” alikumbuka.

Baada ya miaka kusonga sana, ajuza huyo alihisi kutaka kupata mwanaume wa kuishi naye kama mumewe kwa sababu wengi wa marafiki zake kipindi hicho walikuwa wameolewa, lakini hakuweza kufanikiwa kupata mwanaume licha ya juhudi zake.

“Kufikia muda nilikuwa na hisia za kutaka mume wa kunioa, nilikuwa tayari nimepita ujana wangu. Nilikuwa nimezeeka na hilo liliwazuia wanaume kutonikaribia kunitongoza,” alisema.

Ajuza huyo licha ya umri wake kwenda sana, bado ana Imani kwamba siku moja atampata mwanamume wa kumpa joto kabla ya kipindi chake kwenye jukwaa la maisha kufungwa rasmi na Mungu.

“Kusema kweli bado sijakata tamaa kama nitapata mtu anayevutiwa kwangu. Nikipata mtu kama huyo siwezi poteza muda. Najua kwamba umri wangu ni kizuizi kikubwa kwa wanaume wengi lakini nimekataa kukata tamaa hadi pale nitampata mume mzuri. Kwa hiyo kwa wakati huu mimi naona kama mnaweza kunitafutia mwanamume,” alisema.