Nameless: Siwezi zaa mtoto mwingine tena, nimeshafaya vasektomia

Baba wa mabinti watatu alisema kuwa anashangaa sana na fikira za kizamani kutoka kwa watu waliokuwa wakimwambia kuwa anafaa kutafuta mtoto wa kiume.

Muhtasari

• Msanii huyo wa muda mrefu alisema kuwa amesharidhika na mabinti watatu wala hana mpango wa kutafuta mtoto mwingine.

• "Kusema kweli huwa nashangaa sana kwamba watu bado wanaweza niona katika njia za kizamani za kufikiria" - Nameless.

Nameless afichua kuwa alifanya vasektomia.
Nameless afichua kuwa alifanya vasektomia.
Image: Instageam

Msanii mkongwe wa kizazi kipya nchini Kenya, Nameless ambaye ni baba wa mabinti watatu amefichua kwamba hawezi kuzaa mtoto mwingine tena, akiema ameshafanya mchakato wa upangaji uzazi kwa wanaume, Vasektomia.

Akizungumza na mwanablogu Vincent Mboya katika uzinduzi wa mradi wa Talanta Hela katika ikulu ya Nairobi, alisema kuwa hana mpango wa kupata mtoto mwingine tena na hivyo aliamua kuchukua majukumu ya kupanga uzazi mikononi mwake.

“Tushafunga, nimeenda vasektomia. Niliona nichukue majukumu mikononi mwangu. Tumefunga. Kwa wakati huu niliona watoto watatu wa kike wako sawa na tunahisi kubarikiwa sawa, Shiru [binti kitinda mimba] anatuweka bize,” alisema.

Msanii huyo ambaye ni mume wa msanii mwingine nguli, Wahu alisema kuwa michambo ya watu mitandaoni pamoja na shinikizo la kupata mtoto wa kiume wala havimpi presha yoyote.

“Maneno ya watu wala hayana nafasi katika maamuzi yangu, kusema kweli huwa nashangaa sana kwamba watu bado wanaweza niona katika njia za kizamani za kufikiria. Mradi uko na mtoto na ana afya, unafanya jitihada zako zote, hata kama ni asilimia 100, wewe kama mzazi unafaa kuwa kielelezo na mwongozo kwa mtoto,” Nameless alisema.

 Nameless pia alipata nafasi ya kuzungumzia jinsi watu walihisi alipoonesha sura ya mtoto wake mwenye umri wa miezi minane mitandaoni saa chache tu baada ya kuzaliwa.

Alisema kuwa walijawa na furaha na hawakupata fikira kwamba wangeweza kuficha sura yake na pia kusema kuwa bado wanaendelea kujifunza jinsi watu wanakaa mitandaoni kwa kuwa hawakuanza kama wabunifu wa maudhui bali walianza kama wasanii.

“Watu kwa nini walikasirika? Unajua sisi tunajifunza na unajua sisi hatukuanza kama wakuza maudhui, lakini pia sisi tunajua kwamba watu wanapenda kufuatilia safari ya ndoa yetu pia na kwa hivyo tulikuwa tu na furaha na mashabiki wetu na kukashiriki tu,” Nameless alisema.