Hatimaye Diamond amkumbuka Lavalava baada ya kumzimia intaneti kwa muda

Licha ya Lavalava kutoa ngoma kila uchao, hazijawahi sikika na bosi wake hajawahi zipa promo yoyote kwenye kurasa zake mitandaoni kama anavyofanya kwa wasanii Mbosso na Zuchu.

Muhtasari

• Wengi walimsahau kama alikuwepo, kiasi kwamba hata bosi wake Diamond Platnumz kuonekana kumsahau kama alikuwa msanii mwenye mkataba chini ya lebo yake.

Diamond amkumbuka Lavalava baada ya muda mrefu wa kumpotezea
Diamond amkumbuka Lavalava baada ya muda mrefu wa kumpotezea
Image: Facebook

Subira huvuta kheri, ndio pengine methali ambayo wengi wanahisi inamfaa msanii wa muda mrefu ndani ya lebo ya Wasafi WCB, Lavalava.

Msanii huyo katika miaka ya hivi karibuni ametoweka machoni pa mashabiki wa muziki, licha ya kujisatiti na kujitahidi kuachia miziki kila mara, lakini miziki yake imekuwa ikiishia kwenye paa za studio za Wasafi tu!

Wengi walimsahau kama alikuwepo, kiasi kwamba hata bosi wake Diamond Platnumz kuonekana kumsahau kama alikuwa msanii mwenye mkataba chini ya lebo yake.

Diamond aliwekeza nguvu zake nyingi katika promo za wasanii Zuchu na Mbosso ambao kwa sasa wanafanay vizuri, lakini kwa muda hakuwahi kuonekana akifanya udhubutu wa kusukuma kazi za Sanaa za Lavalava, kama ambavyo imekuwa kawaida yake tangu enzi za msanii wake wa kwanza – Harmonize.

Lakini baada ya Lavalava kuachia kibao chake kipya hivi majuzi kinachokwenda kwa jina ‘Tajiri’, bosi wake aliguswa na mapenzi tena, na kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu kumpiga promo hatari Lavalava kwa kupakia kionjo cha kibao hicho.

Diamond aliandika kwamba alikipenda kibao hicho na katika masikio yake kilikuwa kinaimba kwa kujiradidi kama kibwagizo kwenye shairi.

“Kwenye kujirudia rudia #Tajiri na @iamlavalava 🏆” Diamond aliandika.

Itakumbukwa wiki chache zilizopita baada ya Lavalava kushirikishwa na msanii wa muda mrefu kutoka Kenya, Jaguar kwenye kibao cha ‘Unthinkable’, Jaguar alionekana kukisukuma kibao hicho mwenyewe na kwa kurasa za Lavalava wala halikuonekana tangazo hata moja ya promo.

Jaguar alipoulizwa kwa nini, alisema kuwa bosi wa Lavalava – Diamond Platnumz hakuwa ametoa ruhusa kwa kibao hicho kutolewa na Jaguar alichokifanya ni ukaidi tu, jambo ambalo lilimfungia nje Lavalava kutosukuma kibao chao, kwani kipengele cha mkataba wake hakimruhusu kufanya baadhi ya mambo hayo.