Georgina Njenga afichua kumuacha Baha Machachari na kupata mume mwingine

Georgina alimsifia mpenzi wake mpya akisema kuwa penzi analompa ni tofauti ambalo hakuwahi lipata kutoka kwa Baha Machachari.

Muhtasari

• Kwa kuzidisha chumvi kwenye msosi Zaidi, Njenga alisema kwamba hakukawia kwenye soko kwani alitoka kwa Baha hivi na kuruka kwenye uhusiano mwingine.

Georgina Njenga afichua kuachana na Baha Machachari
INSTAGRAM Georgina Njenga afichua kuachana na Baha Machachari
Image: Moses Sagwe

Mpenzi wa muigizaji Tyler Mbaya maarufu kama Baha Machachari, Georgina Njenga ameweka wazi kwamba walishatengana na muigizaji huyo siku nyingi zilizopita.

Njenga alifichua haya katika kipindi cha maswali na majibu na mashabiki wake kupitia Instagram ambaye mmoja alimuuliza kama kweli wako pamoja ama walitengana.

Mlimbwende huyo alijibu moja kwa moja bila kupepesa kwamba ni kweli waliachana na Baha Machachari siku nyingi tu zilizopita.

Kwa kuzidisha chumvi kwenye msosi Zaidi, Njenga alisema kwamba hakukawia kwenye soko kwani alitoka kwa Baha hivi na kuruka kwenye uhusiano mwingine bila kuharibu muda.

“Wewe na Tyler Mbaya kweli mko pamoja ama mliachana kama ambavyo niliona kwa blogu moja?” shabiki aliuliza.

“Hapana… tulishatengana. Watu wengi mmekuwa mkiniuliza hili swali, na hii ndio mara ya mwisho nitalizungumzia. Ni kweli tuliachana, niko katika uhusiano mpya na mwanamume tofauti,” Georgina Njenga alijibu.

Mrembo huyo alimsifia mpenzi wake mpya akisema kuwa mapenzi anayompa ni tofauti kwa kiasi kikubwa na yale ambayo alikuwa anapata kutoka kwa muigizaji huyo wa kipindi kilichokuwa kinapeperushwa kwenye runinga ya Citizen, Machachari.

“Hili ni penzi tofuati kabisa. Sikuwahi kujua kwamba penzi kama hili lilikuwepo. Niko katika sehemu nzuri sasa,” alisema kana kwamba ni kumuonjesha sumu kwa kijiko mpenzi wake wa zamani, Baha.

Wawili hao wana mtoto mmoja pamoja na Georgina Njenga alisema kwamba aliacha kumnyonyesha akiwa na umri wa miezi minane tu.

Ikumbukwe wiki kadhaa zilizopita, Baha alitumbuliwa na nesi kutoka Marekani ambaye alifichua kwamba muigizaji huyo alikuwa amekita kambi kwenye DM yake akiomba hela kwa kisingizio cha kumlea mtoto kumbe alikuwa anazitumia hela hizo katika kuwekeza kwenye mkeka – yaani kucheza Kamari.

Baha siku chache baadae alikiri kwamba alikuwa anapitia wakati mgumu katika maisha ya uraibu, na wadau walijitokeza kumpa shavu na kumliwaza huku wadau wengine wakijitolea kumsaidia katika safari ya kuacha uraibu wa Kamari.